CCM Wanging'ombe Yawaonya Wagombea Watakaotoa Rushwa Ili Kupitishwa Kugombea Udiwani Luduga

 Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Wanging'ombe mkoani Njombe kimewaonya wanaotaka kuteuliwa na chama hicho kugombea udiwani kata ya Luduga kutoshiriki vitendo vya rushwa vinginevyo watachukuliwa hatua za kinidhamu.


Onyo hilo limetolewa leo na katibu wa Chama Cha Mapinduzi wilayani humo Juma Nambaila wakati akitaja wagombea waliopitishwa na chama hicho kugombea nafasi ya udiwani kata ya Luduga.

Amesema wagombea nane wa chama hicho ambao wamepitishwa ngazi ya wilaya kugombea wanatakiwa kufuata miiko na taratibu za uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi ili apatikane atakayeshinda kihalali.

Amesema endapo wakikiuka kanuni zilizowekwa kwa kutoa rushwa ili majina yao yapitishewe na chama hicho kugombea udiwani kata ya Luduga watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Amesema wilaya ya Wanging'ombe ni miongoni mwa kata sita mkoani Njombe ambazo zimetangaziwa kufanya uchaguzi mdogo na mkurugenzi wa tume ya taifa ya uchaguzi ili kujaza nafasi zilizoachwa wazi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo za kifo.

Amesema kata ya Luduga iliyopo wilayani humo inalazimika kuingia katika uchaguzi mdogo baada ya aliyekuwa diwani wa kata hiyo Hassan Ngella kufariki dunia miezi miwili iliyopita.

Amesema chama hicho ngazi ya wilaya baada ya kupokea maagizo kutoka  kiliwatangazia wanachama kata ya Luduga ili kujitokeza kuwania nafasi hiyo ambayo kwasasa ipo wazi.

Amesema wagombea walichukua fomu na kurudisha kati ya tarehe 5 na 6 mwezi huu ambapo wanachama tisa walijitokeza kuchukua fomu ya kugombea udiwani na nane pekee walifanikiwa kurudisha fomu hizo na kukidhi vigezo.

"Tarehe saba mwezi huu tulikuwwa na mkutano maalum wa kura za maoni katika kata ya Luduga ili kuwapigia kura  miongoni mwa hao waliorudisha fomu hizo" amesema Nambaila.

Amesema uchaguzi wa awali umefanyika kwa lengo la kumpata atakayeongoza katika kura za maoni ili vikao vingine vyenye mamlaka ya kutoa maoni na kuteua viweze kukaa na kumpitisha mgombea mmoja atakayepeperusha bendera ya chama hicho.

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi wilayani humo Stephano Kinyangazi amesema kazi ya kamati ya siasa ya wilaya hiyo ni kupitia majina na sifa za wagombea kisha kuyapeleka kamati ya siasa mkoa jambo ambalo tayari limeshafanyika.

Amesema anaamini kamati hiyo ngazi ya mkoa itatekeleza majukumu yake vizuri pasipo shaka kwani wana uzoefu kwakuwa siyo mara yao ya kwanza.

"Tunategemea atakayechaguliwa tutashirikiana pamoja kuhakikisha nafasi hiyo anachukua endapo kitajitokeza chama cha upinzani" amesema Kinyangazi.

Mmoja ya wagombea waliojitokeza kuwania kuteuliwa kuwa mgombea udiwani kata ya Luduga Belshaza Mhanga amesema iwapo chama chake kitampitisha kugombea nafasi hiyo na kushinda kwenye uchaguzi ataanza na ujenzi wa kituo cha afya kwa kushirikiana na wananchi na serikali.

"Kama nitashinda moja kati ya mambo nitakayoanza nayo ni kusimamia ujenzi wa kituo cha afya kwa kushirikiana na wananchi na serikali" amesema Mhanga.

Miongoni mwa wagombea waliopitishwa na chama hicho kuwania kuteuliwa kugombea udiwani kata ya Luduga ni pamoja na Belshaza Mhanga, Andrea Maseleka, Yaledi Mlyuka, Jacob Kilinyi, William Kinywafu, Jaston Chengula, Setti Munganile na Ayoub Fute.
                                 Na Amiri Kilagalila,Njombe

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments