Ile ishu ya Gomes na Simba iko hivi

SIKU chache baada ya Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) kuzuia makocha wasiokuwa na leseni ya UEFA PRO au CAF leseni A, kukaa benchi kwenye mechi za kimataifa na kutaja orodha ya makocha hao akiwamo Didier Gomes wa Simba, Shirikisho la Soka (TFF) nalo limeweka mkazo kwa makocha wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Akizungumza na Mwanaspoti, Boniface Wambura alisema wamefanya marekebisho ya kanuni kuelekea msimu mpya unaoanza Septemba 27, vigezo vimeboreshwa na wanataka kuona kocha mkuu wa timu yoyote awe na leseni A na msaidizi wake B.

Championship League kocha mkuu awe na leseni B msaidizi wake C wakati daraja linalofuata C na msaidizi wake D.

Alisema hata makocha ambao tayari wanadiploma A wataangaliwa na Shirikisho ili kujiridhisha kama kweli ni vyeti vyao sahihi na wanaweza kukidhi mahitaji ndipo wapewe leseni ya kufundisha sio watapitishwa tu kulingana na vyeti vyao.

Alisema CAF na UEFA wamekaa pamoja kupitisha kanuni ya ufundishaji wakakubaliana ili kulinganisha mitaala ili hata leseni wanayoipata Tanzania inaweza kuwasaidia kwenda kufundisha mabara mengine kama Ulaya.

Kuhusu Gomes alisema anatakiwa kupewa muda ili aweze kufuzu mahitaji ya CAF huku akisisitiza ili kupata Leseni A UEFA PRO anatakiwa kusoma mwaka mmoja na kuangaliwa ili kuthibitishiwa kama amepita au arudi tena darasani.

“Sio rahisi sana kama inavyochukuliwa na wengi walichokifanya Simba kumtafuta kocha wa kukaimu nafasi hiyo hawajakosea kwani kocha wao kozi yake ni ya mwaka mmoja na anatakiwa kuangaliwa kwa muda na baadaye kupitishwa kama atakuwa amefanya vizuri,” alisema.

“Diploma A kusoma kwa sasa ni mwaka mzima tofauti na kozi za miezi mitatu au minne kama ilivyozoeleka usomaji wa sasa ni kusoma unafanyiwa uangalizi unaleta ripoti wakufunzi wanakuangalia unaruhusiwa tena kwenda kusoma au kufanya kazi,” alisema.

                            By Charity James

Post a Comment

0 Comments