KATIBU MKUU CHONGOLO AIAGIZA NFRA KUNUNUA TANI LAKI MOJA ZA MAHINDI KUTOKA MIKOA YA NYANDA ZA JUU KUSINI

 CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeiagiza Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kununua tani 100,000 za mahindi katika Mikoa ya Nyanda za juu Kusini mara baada ya awali kukunua tani 24,000 sababu ni kutokana na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania(TMA) kudai kutakuwa na upungufu wa mvua msimu ujao wa kilimo.


Pia,kimeziagiza Wizara za Kilimo na Fedha na Mipango wakutane kujadiliana jinsi ya kupunguza bei ya mbolea kutokana na kuwa juu hivyo kumuumiza mkulima.

Akizungumza na Waandishi wa Habar I leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa CCM Daniel Chongolo amesema Julai mwaka huu Sekretarieti ya CCM ilifanya ziara katika Mikoa ya Rukwa,Songwe na Mbeya ambapo walikutana na changamoto ya wakulima kukosa soko la zao la mahindi.

Amesema mara baada ya ziara hiyo waliiagiza Serikali kununua mahindi hayo ambapo ilitoa zaidi ya shilingi bilioni 14 ambazo zilinunua zaidi ya tani 24,000.

Amedai kwa sasa fedha hizo zimeisha na wakulima wanaendelea kuhangaika kutafuta soko la kuuzia mahindi yao.

Kutokana na hali hiyo Katibu Mkuu huyo ameiagiza Serikali kutoa tena fedha na inunue tani 100,000 za wakulima hao kwani wanazotaarifa kwamba msimu ujao wa kilimo mvua zitakuwa chache.

“Tena kwa bei ile ile ya shilingi 500 kwa kilogramu na wafanye zoezi hilo liwe endelevu kwani mamkala ya hali ya hewa imesema kuna changamoto katika mvua za vuli mpaka katika mvua za masika hivyo kutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa chakula,”amesema.

Pia amesema katika ziara hiyo wamejifunza kwamba uchache wa vituo vya kununulia mahindi hivyo ameiagiza NFRA kuweka vituo ambavyo vitakuwa karibu na wakukulima.

“Kuna malalamiko kukatwa fedha katika shilingi 500 tunasema hapana mtu aliyepo Mufindi,Ileje,Mbozi,Nkasi tunataka bei ya mahindi iwe moja kwa wote wa karibu na mbali,”amesema Chongolo.

Katika hatua nyingine,Katibu Mkuu huyo ameziagiza Wizara za Kilimo na Fedha na Mipango wakutane kujadiliana jinsi ya kupunguza bei ya mbolea kutokana na kuwa juu hivyo kumuumiza mkulima.

Amesema kwa sasa bei ya mbolea aina ya Urea imepanda maradufu kutokana na changamoto ya ugonjwa wa Corona ambapo awali ilikuwa shilingi 50,000 mpaka 55,000 lakini kwa sasa ni shilingi 80,000 mpaka 85,000.

“Tunaiagiza Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Wizara ya Fedha na Mipango waanze mchakato wa jinsi ya kuwasaidia wakulima.Nasisitiza Wizara zikutane mapema kuwezesha kupungua kwa bei ya mbolea,”amesema.

Hata hivyo,Katibu Mkuu huyo amesema mara baada ya maagizo hayo baada ya wiki mbili wataanza ziara ya kukagua maelekezo hayo.

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi CCM, Ndugu Daniel Chongolo

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments