Recent-Post

KATIBU MKUU WA CCM ASISITIZA SENSA, MIKUTANO YA MASHINA NA KUWAONYA WALIOANZA HARAKATI MAJIMBONI

 Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amesisitiza umuhimu wa Sensa, mikutano ya Mashina na kuwaacha waliopata dhamana kufanya kazi.


Amezungumza hayo leo tarehe 15 Septemba, 2021 wakati wa Mapokezi ya ziara yake Mkoa wa Lindi akiambatana na Wajumbe wa Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa.

Akizungumzia suala la Sensa ya Watu na Makazi, Katibu Mkuu amewataka viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali  kuhakikisha katika maongezi yao na wananchi wanahamasisha zoezi la Sensa lililozinduliwa na Rais wa Tanzania na Mwenyekiti wa CCM Mhe. Samia Suluhu Hassani Jijini Dodoma, ambalo linatarajiwa kufanyika Mwaka 2022,  kwani Sensa  ndio msingi wa maendeleo ya nchi na uchumi wetu.

"Sensa katika nchi ndio Uchumi  na ndio Maendeleo, tukitengeneza  mazingira  mazuri  ya kuhamasishana  na kujitokeza  vya kutosha  katika kushiriki Sensa zoezi  ambalo limezinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Dodoma, tutaipa serikali fursa ya kupanga Mipango ya Maendeleo kwa urahisi na kufikia maendeleo yenye usawa na kwa haraka." Katibu Mkuu amesisitiza

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amewaonya watu wanaofuatilia nafasi za ubunge na udiwani wanapaswa kuacha mara moja, kwani Uchaguzi umeshapita na CCM haiwezi kuwa Chama cha  Uchaguzi wakati wote badala ya kuwaletea wananchi maendeleo.

"Kama unapenda Ubunge ama udiwani subiri 2025 sasa hivi chokochoko  katika majimbo zinatoka wapi,na chokochoko za nafasi zinatoka wapi..?waacheni wabunge wafanye kazi  wanazofanya, subirini 2025, tukihangaika kuwafuatilia sasa hivi na kuwazushia uongo tutafika mwaka 2025 na majeraha makubwa." Katibu Mkuu ameeleza

Ameongeza kuwa, "Kila mtu anahaki  ya kutumia nafasi yake ya uanachama ndani ya Chama hiki kugombea, lakini hana haki ya kumsumbua aliyeshinda uchaguzi kwa kuwa tuna kazi ya kujenga nchi na  kutekeleza Ilani ya Chama chetu."

Akizungumzia Uhai wa Chama Mashinani, Katibu Mkuu amesema,  katika uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama unaotarajiwa kufanyika mwakani, mtu akitaka kuchagulia kuwa Kiongozi ndani ya Chama ni lazima awe amehudhuria mikutano ya  mashina. Mwanachama hawezi kuwa Kiongozi wa Chama kama hakushiriki mikutano ya Mashina kwa ushahidi wa mihutasari.

Akiendelea na Ziara Wilayani Kilwa Katibu Mkuu ametembelea na kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha Chumo na kuhudhuri mkutano wa Shina namba 3 Tawi la Chumu Kata ya Chumo.

Huu ni muendelezo wa Utekelezaji wa Maelekezo ya Kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa cha  tarehe 29 Juni, 2021ikiwa ni  kuimarisha Uhai wa Chama katika ngazi za Mashina pamoja na Kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 - 2025.Post a Comment

0 Comments