Kikwete amzungumzia Rais Samia



Miezi sita tangu Rais Samia Suluhu Hassan aanze kuiongoza Tanzania, Rais Jakaya Kikwete amesema anafanya vema na kuwataka watendaji wa Serikali na wananchi kumpa ushirikiano.

Kikwete aliyekuwa Rais wa awamu ya nne amesema hayo leo Jumanne Septemba 14, 2021 kwenye hafla ya makabidhiano ya eneo la ujenzi wa hospitali ya Halmashauri ya Chalinze utakaogharimu Sh1.2 bilioni huko Msoga.

Ujenzi huo unafadhiliwa na Shirika la Abbott linalojihusisha na masuala ya afya kutoka Marekani.

“Jamani urais sio kazi rahisi, ina mawimbi mengi, inahitaji mtu makini. Mpaka sasa mama Samia ameweza na kwa kipindi kifupi tu tumeona ameendesha nchi vizuri licha ya changamoto zilizopo,” amesema Kikwete.

Kuhusu mradi huo, Rais Kikwete aliyemaliza muhula wake mwaka 2015 amesema alianza kushirikiana na Abbott tangu akiwa madarakani.

“Mradi huu wa Msoga mimi nimesaidia tu kwa sababu natambua kuwa utaokoa  maisha ya waathirika wa ajali mbalimbali zinazotokea Barabara Kuu ya kutoka Chalinze kwenda Segera na kutoka Chalinze kwenda Morogoro,” ameeleza Kikwete.

Hata hivyo, ameshauri Serikali itoe mafunzo ya matibabu ya dharura kwa watumishi wa afya ili wapatikane wabobezi wa huduma hiyo.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel aliyehudhuria makabidhiano hayo ameipongeza Halmashauri ya Chalinze kwa namna wanavyotumia vizuri fedha za Serikali zinazopelekwa kujenga vituo vya afya kwenye halmashauri hiyo.

Dk Mollel amesema Sh400 milioni zilizopelekwa na Serikali kwenye kila wilaya kujenga vituo hivyo na nyingi zimejenga majengo matatu lakini Chalinze yapo manne.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge ameishuruku Serikali kuutekeleza mradi huo wa huduma za dharura unaotarajiwa kukamilika Septemba mwakani na kuwataka wananchi kuendelea kumpa ushirikiano Rais Samia kusogeza huduma za afya jirani na wananchi.

                                                Chalinze. By Julieth Ngarabali

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments