KITUO CHA UTAMADUNI UFARANSA JIJINI DAR CHAWAKUTANISHA WADAU SEKTA YA SANAA

 UBALOZI wa Ufaransa nchini Tanzania kupitia Kituo chake cha Utamaduni kilichopo jijini Dar es Salaam umekuwatanisha wadau wa sanaa kutoka nchi za Afrika Mashariki kujadiliana kwa kina kuhusu kukuza ubunifu kwenye sekta ya sanaa.


Wakati wa majadiliano hayo wadau hao wa sekta ya sanaa wamejadili kwa kina mbali ya kukuza na kuendeleza ubunifu ni jinsi gani wasanii wanaweza kujihusisha katika kufanya biashara kupitia sanaa hiyo hasa kwa kutambua sekta ya sanaa imekuwa ikitengeneza mabilioni ya fedha katika nchi mbalimbali ikiwemo nchi ya Ufaransa.

Akizungumza kabla ya kuanza kwa majadiliano hayo Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui ambaye amewasili nchini hivi karibuni na anasubiri kupokelewa rasmi na Serikali ya Tanzania , ametumia nafasi hiyo kueleza kwa kifupi mchango wa sanaa unavyoweza kukuza na kuimarisha uchumi.

Hivyo ameeleza namna ambavyo nchi ya Ufaransa inavyotambua na kuthamini sekta hiyo na imekuwa ikiipa kipaumbele."Tukio hilo leo ndio la kwanza kwa upande wangu, ingawa najua kazi kubwa ambayo inafanywa na nchi yetu ya Ufaransa kuhakikisha sekta ya sanaa inapewa kipaumbele.

"Tutaendelea kushirikiana na nchi za Afrika ikiwemo nchi za Afrika Mashariki katika kuifanya sanaa inakuwa sekta endelevu na kuinua maisha ya wasanii kiuchumi,"amesema Hajlaoui.

Awali Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa(Alliance Francaise)jijini Dar es Salaam Flora Valleur amesema kituo hicho kitaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya sanaa kuhakikisha sanaa inaendelea kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya vijana.

"Nchi ya Ufaransa imekuwa ikiwekeza zaidi katika kusaidia eneo la sanaa kwa kutambua kuwa eneo hilo ni moja ya eneo ambalo linaingza fedha nyingi , kule Ufaransa sekta ya sanaa inaingiza faida ya EUR bilioni 100 kwa kila mwaka huu, faida ambayo ni kubwa kuliko hata biashara ya magari,"amesema.

Ameongeza nchini Ufaransa kuna watu 670,000 ambao wanafanya kazi katika sekta ya sanaa, hivyo Ubalozi wa Ufaransa nchini Tanzania kupitia kituo hicho utaendelea kutoa kila aina ya ushirikiano kwa wasanii wa Tanzania na Afrika Mashariki katika kufikia malengo ya kuikukuza sanaa hiyo.

Amefafanua kuwa kituo hicho kina kazi kuu mbili , kwanza kufundisha lugha ya Kifaransa ambayo ni miongoni mwa lugha zinazozungumzwa katika nchi mbalimbali duniani, lakini kazi ya pili ni kazi nyingine ya kituo hicho ni kuendeleza sanaa na utamaduni."Kutokana na changamoto ya Corona tulisimama kidogo lakini sasa angalau hali imeanza kuwa nzuri, hivyo tutaanza tena maonesha ya muziki wa live kila siku ya Jumatano kuanzia Oktoba mwaka huu na tunatarajia kuandaa matamasha ya maonesho ya kazi za sanaa."

Kwa upande wake Mchekeshaji na mtangazaji Evance Bukuku amesema mdahalo huo wa sanaa umekuja wakati muafaka na hasa katika kuangalia sanaa inavyoweza kutumika kuwa biashara."Wasanii wamepitia magumu katika sanaa lakini sasa tunataka kuitumia sanaa kama barabara ya kwenda katika biashara, hivyo majadiliano haya ya leo ni muhimu."

Ameongeza wana kila sababu sababu ya kuangalia sanaa kuwa kazi na biashara, lakini huwezi kupita njia ya mkato, kwa hiyo kupitia mdahalo huo unaiotwa Tuongee kuhusu ubunifu wasanii watapata mbinu za kuifanya sanaa yao kuwa biashara.

Wakati huo huo mwanamuziki kutoka nchini Kenya Muthon Dramer Queen amesema sekta ya sanaa kwa Afrika Mashariki imebeba kundi kubwa la vijana na kwa upande wake anaiona sanaa kama kiwanda kikubwa cha kuzalisha wasanii na kazi za wasanii."Thamani ya sanaa inaendelea kukuwa na wasanii wa Afrika Mashariki tutafanya makubwa zaidi kupitia kazi zetu za sanaa."

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui akizungumza na wadau wa sekta ya sanaa kabla ya kuanza kwa mdahalo uliohusu kujadili jinsi ya kukuza ubunifu kwenye sekta hiyo.Mdahalo huo umefanyika Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi na Rocky Star Afrika Seven Mosha(katikati) akifafanua jambo wakati wa mdahao huo.Kushoto ni Mwanamuziki Muthon Dramer Queen, kutoka nchini Kenya na mchoraji maarufu nchini Asteria Malinzi(kulia).

Mmoja ya wasanii wa uchoraji akiendelea na majukumu yake ya kuchora wakati mdahalo huo uliohudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya sanaa ukiendelea katika Kituo cha Utamaduni cha Ubalozi wa Ufaransa jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Kituo cha Utamaduni cha Ufaransa(Alliance Francaise)jijini Dar es Salaam Flora Valleur akifafanua jambo kuhusu kituo hicho kinavyoriki kikamilifu katika kukuza utamaduni na sanaa.

Sehemu ya wadau wa sanaa waliohudhuria majadiliano yaliyohusu kukuza na kuimarisha sekta ya sanaa.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui akisisitiza jambo kuhusu nchi yake ambavyo imejipanga kushirikiana na nchi za Afrika Mashariki katika kuendeleza sekta ya sanaa na utamaduni.

Msanii wa Bongo Fleva Ben Paul (katikati) akijitambulisha kwa Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui(kushoto).Balozi Nabil amekuja nchini siku za karibuni akichukua nafasi iliyoachwa na Balozi aliyemaliza muda wake na tayari ameshaondoka nchini.

Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania Nabil Hajlaoui(kulia) akiwa na mkewe Amna Hajlaoui(kushoto) wakati wa majadiliano hayo ya kuhusu kukuza sekta ya sanaa 

Mchekeshaji na Mtangazaji Evance Bukuku (kulia) akimuliza swali mchoraji maarufu nchini Asteria Malinzi(wa pili kulia) wakati wa majadiliano hayo.Wengine kuanzia kushoto ni mwanamuziki Muthon Dramer Queen kutoka nchini Kenya na Mkurugenzi na Rocky Star Afrika Seven Mosha.
Na Said Mwishehe, Michuzi TV

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments