Kusuasua ujenzi wa barabara Butiama kwamuibua Mama Maria Nyerere

Butiama. Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara amemwonya mkandarasi anayejenga barabara ya Makutano - Sanzate wilayani Butiama mkoani Mara, akisema imeshusha heshima ya Serikali katika kumwenzi Hayati Mwalimu Julius Nyerere kwa sababu ya kuchelewa kumaliza.

Waitara ametoa kauli hiyo leo Septemba 19 alipotembelea barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 50, akisema kutokana na ucheleweshaji huo, Mama Maria Nyerere aliamua kufuatilia ili kujua kulikoni kutokana na barabara hiyo kugeuka kuwa kero kwa wakazi wa wilaya hiyo.

"Baada ya kuona mradi unasuasua Mama Maria aliamua kufuatilia yeye mwenyewe ili kujua kuna shida gani maana mradi umechukua muda mrefu. Hivi hii ni haki kweli mama Maria anafanyakazi ya kufuatilia mradi badala ya kukaa nyumbani apumzike?

“kwakweli mmeshusha heshima ya serikali lakini pia imani ya serikali kwenu ninyi wakandarasi wazawa pia imeshuka," amesema Waitara

Amesema kuwa serikali iliamua kuwapa kazi kwa wakandarasi wazawa ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza miradi mikubwa, badala ya miradi hiyo inatekelezwa kwa kiwango cha chini.

"Yaani hata mradi wa Sh30 bilioni tunalazimika kuwapa wakandarasi kutoka nje kwasababu ya mambo kama haya, hapa kulikiwa na muungano wa wakandarsi 10 lakini wamekimbia amebakia mmoja tu sasa unategemea nani atawapa kazi tena?" amehoji Waitara

Awali Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads) mkoa wa Mara,  Felix Ngaile alisema kuwa barabara hiyo iliyoanza kujengwa mwaka 2013 ilitarajiwa kukamilika mwaka 2015 lakini hadi sasa haijakamilika kutokana na changamoto kadhaa ikiwemo ucheleweshaji wa malipo.

Amesema kuwa hadi sasa mradi huo umefikisha asilimia 90 na kwamba unatarajiwa kukamilika Desemba mwaka huu na kwamba hadi kukamilika mradi huo unatarajiwa kugharimu zaidi ya Sh 60 bilioni na kuongeza kuwa mkandarasi tayari amenunua vifaa kwaajili ya kukamilisha mradi huo.

Agosti Mkandarasi alilipwa madeni aliyokuwa akidai na tayari ameleta mtambo wa kusaga kokoto wenye uwezo wa kuzalisha tani 250 kwa saa, pia ameshanunua vifaa vilivyokuwa vinahitajika kama vile lami na saruji hivyo tumekubaliana kazi hii ikamilike Desemba ili iweze kukabidhiwa serikalini tayari kwa matumizi," amesema Ngaile.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments