Recent-Post

LIGI INAANZA, WACHEZAJI KAZI IENDELEE, WAAMUZI SHERIA 17


LIGI Kuu Bara leo inatarajiwa kuanza kwa timu kuanza kuonyesha kile ambacho inacho na inahitaji nini kwa msimu mzima hivyo ni msingi kila mmoja akajipanga kwa ajili ya kupata matokeo chanya.

Mechi nyingi ambazo zinachezwa nina amini kwamba zitakuwa zinaushindani mkubwa jambo ambalo litaleta mvuto wa kuzitazama na kuzifuatilia.

Tunachokihitaji ndani ya ligi kwa sasa ni ushindani kwa sababu kukiwa na ushindani kunafanya kila timu iamini kwamba ipo imara na inaweza kuleta ushindani kwa mpinzani.

Ushindani utasaidia kukuza ligi na kufanya kuwa na timu ya Taifa ya Tanzania ambayo ni imara na itaweza kufanya vema kwenye michuano mbalimbali kimataifa.

Jambo hilo litasaidia kuuza wachezaji wa ndani nje ya nchi jambo ambalo litafanya soka letu kuwa bora na kuzidi kuleta ushindani kwa mataifa mengine ambayo yameendelea.

Ili kuwa na ligi makini pamoja na timu ya Taifa bora ni lazima uwe na wachezaji wengi ambao wanajituma na kufanya vizuri ndani ya uwanja.

Kwa kufanya hivyo ikiwa itatokea wachezaji wengi watauzwa nje ya nchi itaongeza ushindani kwa mchezaji mmojammoja ndani ya timu kiujumla na endapo atapata nafasi ya kuitumikia timu ya taifa basi imani yetu ni kwamba ataonyesha utofauti.

Timu zote ndani ya ligi shiriki ikiwa zitacheza kwa kupambana, hili ni muhimu kuzingatia kwani mashabiki wanapenda kuona timu ikipata matokeo chanya uwanjani.


Kwa sasa tunaamini kwamba  timu zitakuwa zinashinda ugenini pia jambo ambalo lilikuwa linaonekana kuwa gumu kwa msimu uliopita ila kwa sasa mambo nina amini yatabadilika.


Kila timu na ipambane kufanya vizuri kwenye mechi zake ili kupata matokeo kwa kuwa hakuna kinachohitajika ni matokeo mazuri na inawezekana.


Mbeya City wakiwa nyumbani ama Namungo pia wakiwa nyumbani wanaweza kupoteza kwa kuwa ligi ni ushindani hakuna ambaye hawezi kufungwa hilo liwe kwenye akili za mashabiki pamoja na wachezaji.


Mechi nyingi ambazo zitaonyeshwa na Azam TV nina amini kwamba zitakuwa na mvuto wa kipekee na zinaonekana zitakuwa tofauti jambo ambalo linatarajiwa kuwa hivyo msimu mzima.


Hii iwe ni fursa kwa wachezaji kuitumia kuuza uwezo wao nje ya nchi  kwa kuwa ligi ya Tanzania kwa sasa inafuatiliwa na wengi duniani ukizingatia kwamba mechi zote za Ligi zitarushwa mubashara ndani ya Azam TV.


Kwa upande wa waamuzi nao wanatambua majukumu yao ni kufuata sheria 17 za mpira nina amini itakuwa hivyo kwa kuwa wamekuwa wakifundishwa namna ya kusimamia sheria.


Kila mmoja atimize majukumu yake kwa kuwa kinachohitajika ni ushindi na imani yetu ni kwamba msimu wa 2021/22 utakuwa na ushindani mkubwa na inawezekana kila mmoja akatimiza majukumu yake.

Post a Comment

0 Comments