LUIS,CHAMA WAANZA KUSAHAULIKA SIMBA

 

NYOTA wapya waliosajiliwa Simba wameanza kuonyesha uwezo wao ambao utawafanya mashabiki wao kuwasahau Clatous Chama na Luís Miquissone waliouzwa hivi karibuni.

Nyota hao Saido Kanoute, Ousmane Sakho na Peter Banda walikuwa wakisubiriwa kwa hamu zaidi na wadau wa soka kuona kama wataweza kufiti katika nafasi zilizoachwa na nyota hao ambao walitoa mchango mkubwa msimu uliopita.

Nyota hao walicheza mechi ya kirafiki ya kimataifa dhidi ya TP Mazembe siku ya kilele cha Simba Day na Simba kufungwa bao 1-0, Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.

Nyota wa zamani wa timu hiyo, Amri Kiemba alisema mashabiki wa soka nchini wasiwafananishe wachezaji walioondoka na waliopo sasa kwani kila mchezaji ana ubora wake.

“Tusilazimishe kuwapata kina Chama na Luís na wachezaji wengine kwani kila mchezaji ana ubora wake wa kipekee ambao wachezaji wengine hawawezi kuwa nao uwanjani.

Ukiangalia safu ya kiungo ya Simba iliyoanza kwenye mchezo huo ikiongozwa na Lary Bwalya ilijaribu kuja na kitu tofauti katika upishi wa mabao na hii ni kutokana na aina ya uchezaji wa Bwalya anapokuwa na mpira,” alisema Kiemba.

Alisema bado Simba wana nafasi ya kuwatumia nyota wapya na waliokuwepo ndani ya kikosi hicho kupata radha mpya ya upikaji wa mabao.

Sijaona mabadiliko sana ndani ya Simba katika mechi hiyo, kikosi kilichoanza japokuwa wamesajili wachezaji zaidi ya 10 msimu huu hivyo naona kocha bado ana nguzo yake ambayo hadi sasa ipo na anaendelea kuitumia hivyo inatoa tafsiri kuwa Didier Gomez anaweza kukiboresha zaidi.”

Kwa upande wa Musa Mgosi alisema; “Simba hatuna pengo kwani tuna wachezaji wazuri sana ambao wanaweza kuifanya kazi kwa ubora wao hivyo hakuna sababu sababu ya kuendelea kuwafikiria wachezaji waliondoka.”

Kocha msaidizi wa Simba Queen, Matty Msati alisema; “Bado kuna kazi ya ziada sana kuyaziba mapengo yalioachwa na Luis na Cham hasa ukiangalia jinsi safu ya kiungo ilivyopata shida katika mchezo na Mazembe kwenye kutengeneza nafasi za mabao kazi ambayo nyota hao waliifanya na matokeo chanya.”

Simba inatarajia kuingia dimbani kucheza mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga, Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa.

Mara ya mwisho timu hizo zilikutana mechi ya fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) na Simba kutwaa ubingwa huo kwa bao 1-0. Fainali ilichezwa Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

         By LEONARD MUSIKULA

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments