Mambo yaliyotokea Rugemalira akiwa jela


 Mfanyabiashara James Rugemalira, huenda leo akawa miongoni mwa waumini wa Kanisa Katoliki Parokia ya Makongo Juu, Dar es Salaam, watakaoshiriki huduma za kiroho kanisani hapo.

Rugemalira, ambaye amefutiwa kesi ya uhujumu uchumi iliyomfanya kukaa gerezani kwa siku 1,550 kabla ya kuachiwa huru Ijumaa, ni muumini wa kanisa hilo na hata muda mfupi baada ya kukamilisha taratibu za kutoka kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, moja kwa moja alifika kanisani hapo kwa ajili ya kumshukuru Mungu akiwa na familia yake.

Akiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya Asia, Harbinder Singh Sethi, walikamatwa na kufikishwa mahakamani Juni 19, 2017 na kuanzia hapo, walikaa rumande mpaka Juni 16, mwaka huu, Sethi alipoachiwa.

Sethi aliachiwa baada ya kufanya makubaliano na Mkurugenzi wa Mashitaka wa Serikali (DPP), akiridhia kulipa Sh26 bilioni.

Kwa mujibu wa hesabu, tangu Rugemalira alipokamatwa na kuwekwa mahabusu, ilipita miaka mitatu, miezi minane na siku 26, huku matukio mbalimbali yaliyotikisa nchi yakitokea, ikiwamo kifo cha Rais John Magufuli, wakati huo akiwa ameshatumikia siku 1,358 akiwa mahabusu.

Ukiacha kuzikosa siku 1,358 za urais wa Magufuli na 181 za Samia, Rugemalira, katika kipindi alichokaa mahabusu alipitwa na mengi, ikiwamo tukio la Makamu Mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara, Tundu Lissu kushambuliwa kwa risasi Septemba 7, 2017.

Wakati Lissu aliposhambuliwa, Rugemalira alikuwa ndio anatimiza miezi miwili na siku 19, tangu alipoanza maisha ya mahabusu. Hivyo, bila shaka alilisikia tulio hilo akiwa nyuma ya nondo.

Kuanzia Desemba 2, 2017 hadi mwanzoni mwa mwaka 2020, wabunge wa upinzani walitangaza mfululizo kujiondoa kwenye vyama vyao na kuhamia CCM, kwa hoja ya kuunga mkono juhudi za Dk Magufuli. Hamahama hiyo, Rugemalira aliisikia akiwa mahabusu.

Wakati alipokamatwa, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alikuwa Paul Makonda, ametoka na kukuta jiji hili kubwa kibiashara nchini na Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, likiongozwa na Amos Makalla, na alishapita Abubakar Kunenge, ambaye Rugemalira amemkuta akiwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani.


Vifo

Ukiacha kifo cha Magufuli, vimetokea vifo vingi tangu maisha ya Rugemalira yalipohamia mahabusu. Rais wa tatu, Benjamin Mkapa, alifariki dunia Julai 24, 2020, akiwa tayari ana miaka mitatu, mwezi mmoja na siku tano mahabusu.

Kabla ya Rais Mkapa, Tanzania iliingia kwenye historia ya kuwapoteza wabunge wengi ndani ya kipindi kifupi. Ndani ya siku 11, wabunge watatu walifariki dunia mwaka 2020.

Aliyekuwa mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Morogoro (CCM), Gertrude Rwakatare alifariki dunia Aprili 20, mwaka jana. Rwakatare pia alikuwa Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Mikocheni B Assemblies of God, maarufu Mlima wa Moto.

Siku tisa baada ya kifo cha Rwakatare, aliyekuwa Mbunge wa Sumve (CCM), Richard Ndassa alifariki dunia. Ndassa alifikwa na mauti Aprili 29, mwaka jana. Kisha, Mei Mosi, yaani siku moja baada ya Ndassa kufariki, aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria na mbunge wa kuteuliwa, Augustine Mahiga alifariki dunia.

Soma hapa: Rugemalira atoa sadaka ya shukrani kanisani

Vifo zaidi vilivyotokea kipindi Rugemalira akiwa mahabusu ni cha aliyekuwa mjumbe wa Baraza la Mawaziri la kwanza la Mwalimu Julius Nyerere, Balozi Job Lusinde, vilevile Mwanasheria Mkuu wa kwanza mzawa, Mark Bomani.

Aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif Sharif Hamad, aliyekuwa Katibu Kiongozi, Balozi John Kijazi, wote hao vifo vyao vilimkuta Rugemalira akiwa mahabusu.

Uchaguzi Mkuu 2020, kampeni na ulivyofanyika, Rugemalira alisimuliwa akiwa mahabusu. Vilevile Taifa lilivyovuka kipindi chenye changamoto, cha makabidhiano ya urais, kwenda kwa Rais Samia Suluhu Hassan baada ya kifo cha Magufuli, nacho kilipita akiwa mahabusu.

Machi mwaka jana ilitokea sinema ya siasa za Mahakama, baada ya viongozi wa juu wa Chadema kukutwa na hatia, hivyo kutakiwa kukaa jela miezi mitano au kulipa faini.

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu, John Mnyika, aliyekuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake Chadema (Bawacha), Halima Mdee, walikuwa ni sehemu ya viongozi waliokutwa na hatia katika kesi ya kusababisha kifo cha aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.

Wengine ni Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa, aliyekuwa mbunge wa Tarime, John Heche, wabunge wa viti maalum, Esther Matiko na Ester Bulawayo, vilevile aliyekuwa Katibu Mkuu, Vincent Mashinji.

Tukio la viongozi hao kuhukumiwa, lilisababisha kuibuka kwa hamasa kubwa ya michango kutoka ndani na nje ya nchi, hivyo kufanikisha kupatikana kwa fedha nyingi, zilizowezesha wote kutolewa. Sinema hiyo, Rugemalira hakuishuhudia.

                                             By Luqman Maloto

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments