Recent-Post

MBUNGE ASIA AONGOZA HARAMBEE NA KUPATIKANA SHILINGI MILIONI 6 ZA NYUMBA YA UVCCM SIMANJIRO

MBUNGE wa Vijana Taifa kupitia Mkoa wa Manyara, Asia Halamga ameongoza harambee ya kukusanya fedha za ujenzi wa nyumba ya Katibu wa UVCCM Wilayani Simanjiro na kufanikisha kupatikana kwa shilingi milioni 6.9


Asia ameongoza harambee hiyo iliyofanyika jana mji mdogo wa Mirerani kwenye kikao cha baraza la UVCCM Wilayani Simanjiro, ambapo fedha taslimu zilipatikana shilingi milioni 2.8 na ahadi shilingi milioni 4.1

Hata hivyo, Mbunge huyo Asia amewaahidi vijana hao kuwa atafanikisha gharama ya kufunga nyaya za umeme pindi nyumba hiyo ya katibu wa UVCCM wilaya ya Simanjiro ikifikia hatua hiyo.

“Huu siyo mwisho wa kushirikiana nanyi kwani Simanjiro mmekuwa bega kwa bega nami hivyo tutaendelea kuungana mkono kwenye maendeleo bila wasiwasi wowote ule, amesema Asia.

Mbunge wa jimbo la Simanjiro, Christopher Ole Sendeka amempongeza Asia kwa namna anavyomuunga mkono Bungenni kutetea maslahi ya wana Simanjiro.

“Tunapaswa kumkumbuka Asia kwa moyo wake wa upendo kwani alilia nasi Bungeni kipindi cha wadau wa madini wapekuliwa bila staha, waswahili wanasema mnyonge mnyongeni ila haki yake mpeni,” amesema Ole Sendeka.

Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Simanjiro, Baraka Kanunga amewapongeza viongozi wa UVCCM wa wilaya hiyo kwa dhamira ya ujenzi wa jengo hilo.

Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Thomas Mollel amemshukuru Mbunge huyo Asia kwa kufanikisha harambee hiyo ya ujenzi wa nyumba ya mtumishi wao wa wilaya yao.

Katibu wa UVCCM Wilaya ya Simanjiro, Bakari Mwacha amesema ujenzi wa nyumba hiyo utaendelea wiki ijayo kwani harambee hiyo imefanikisha fedha zitakazonunua vifaa.

Mjumbe wa Halmashauri kuu ya CCM Mkoa wa Manyara, Kiria Laizer amesema anachangia shilingi milioni 2 kwani jumuiya hiyo imemlea akiwa Mwenyekiti wa Wilaya hiyo kwa miaka miwili na alishachangia ujenzi wa ofisi pia.

         Na Mwandishi wetu, Simanjiro

Post a Comment

0 Comments