Mfahamu aliyeongoza mapinduzi Guinea

(AFP). Luteni Kanali Mamady Doumbouya, kiongozi wa mapinduzi nchini Guinea, ni msomi wa hali ya juu, mwanajeshi mtaalamu wa vita ambaye wakati fulani aliwahi kufanya kazi na jeshi la wageni nchini Ufaransa.

Jumapili, kikosi maalum cha Doumbouya kilimpindua Alpha Conde, kiongozi wa taifa hilo la magharibi mwa Afrika mwenye umri wa miaka 83 ambaye awali alipigania demokrasia lakini baadaye akatuhumiwa kwa kuongoza nchi kimabavu.

Mwanasiasa huyo mkongwe alikuwa rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia mwaka 2010 baada ya kukaa gerezani kwa miaka kadhaa alikofungwa na wanamapinduzi waliopita.

Lakini mwaka jana alikasirisha watu alipofanya mabadiliko ya katiba yaliyomuwezesha kugombea tena urais kwa kipindi cha tatu.

Akiwa amevaa kibandiko cha kijeshi kichwani na miwani ya jua, Doumbouya alitangaza kufuta katiba, ambayo mabadiliko yake yalimuwezesha Conde kupata kipindi cha tatu cha urais katika uchaguzi uliopingwa vikali.

Baadaye, akiwa amejifunika bendera ya taifa bila ya kuvaa miwani, Doumbouya aliahidi kuongoza "mabadiliko jumuishi na ya amani".
Kumekuwepo na vifo vingi bila ya sababu, wengi wamejeruhiwa, wengi kutoka machozi," alisema, akirejea vitendo vya Conde vya kudhibiti maandamano na kusababisha umwagaji damu.

Ili aeleweke fikra zake, Doumbouya ameibua kumbukumbu za kiongozi wa zamani wa Ghana, Jerry Rawlings, ambaye aliingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1981 kabla ya kuongoza mabadiliko ya kuelekea demokrasia.

Kama watu wanapigwa na watawala, ni jukumu la jeshi kuwapa watu uhuru," alisema Doumbouya, akimkariri Rawlings.

Mtu huyo aliyeanza kudokolewa macho ni ofisa ambaye ndio kwanza amefika umri wa miaka kuanzia 40 na ambaye alipata shahada ya umahiri katika ulinzi Chuo Kikuu cha Pantheon-Assas jijini Paris.

Alipata mafunzo ya kijeshi kutoka Chuo cha Ecole Guerre nchini Ufaransa na alikuwa kwenye Jeshi la Foreign Legion, ambalo huruhusu raia wa kigeni wanaotaka kuingia jeshi la Ufaransa.
Akiwa mwanajeshi, ameshashiriki operesheni nchini Afghanistan na katika nchi yenye matatizo ya Jamhuri ya Afrika ya kati.


Kikosi chake, Kikundi Maalum cha Jeshi, ndio kwanza kilikuwa kimeanzishwa wakati mwaka 2018 wanakikundi walipopiga kwata kusherehekea miaka 60 ya uhuru kikiwa chini ya rais ambaye miaka mitatu baadaye kimekuja kumpindua.

Doumbouya anatoka Kankan mashariki mwa Guinea, na kama Conde anatoka kabila linaloitwa  Mandinka.
Ameoa Mfaransa na ana watoto watatu, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Guinea.


Doumbouya, 41, alianzia kikosi cha Foreign Legion cha Ufaransa, ambako alipanda cheo kuanzia koplo kabla ya kuitwa kuongoza kikosi maalum cha SFG.

Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 15 jeshini ambao unajumuisha kufanya kazi katika operesheni nchini Ivory Coast, Djibouti, Afrika ya Kati, Afghanistan na sehemu nyingine duniani.

Doumbouya ni mtaalamu wa usimamizi wa jeshi, kamanda na mtu wa mikakati akiwa amepata mafunzo ya utaalamu aliyomaliza kwa mafanikio katika Chuo cha Kimataifa cha Usalama nchini Israel, pamoja na mafunzo ya kijeshi nchini Senegal na Gabon.


Pia amewahi kufanya kazi Cyprus, Uingereza na Forecariah, magharibi mwa Guinea ambako alifanya kazi katika kitengo cha usimamizi wa mipaka na ujasusi.

'kujifunza kutokana na makosa'
"Hatujaja hapa kufurahia madaraka, hatujaja kucheza, tutajifunza kutokana na makosa yote yaliyofanyika," alisema katika kituo cha yelevisheni cha Ufaransa, France 24, akirejea mapinduzi yaliyopita ambayo yaliacha makovu kwa taifa.

Kiongozi wa zamani wa mapinduzi ya mwaka 2008-09, Kepteni Dadis Camara, alifurahia kuonekana mara kwa mara katika televisheni hadi kupachikwa jina la "Dadis Show".

Mwezi Septemba 2009, wanajeshi waliua wafuasi wa upinzani waliokuwa uwanjani katika mji mkuu wa nchi hiyo, Conakry. Takriban watu 157 waliuawa, wakati wanawake 109 walibakwa.
Jumapili, Doumbouya alitangaza: "Hatutakubali tena kumuachia siasa mtu mmoja, tutaiweka siasa kwa watu."

Guinea ni nzuri. Hatuhitaji kuibaka zaidi Guinea, tunachotakiwa ni kuipenda."

Doumbouya alikemea rushwa na ubadhirifu, na kuahidi kulinda amani katika nchi hiyo.
Lakini wanadiplomasia na vyombo vya habari vya Guinea wanasema kilichosababisha mapinduzi hayo kinaweza kuwa ni mvutano na serikali kuhusu wizara ya ulinzi kusimamia vikosi maalum vya jeshi.
Mapinduzi ya Guinea ni tukio jipya katika mwenendo wa kuangusha serikali ambao umekuwa ukiendelea barani Afrika katika miaka ya karibuni.


Nchini Mali, Rais Ibrahim Boubacar Keita alipinduliwa Agosti 2020 baada ya maandamano kutanda mitaani.
Mwezi Mei jeshi lilichukua nchi tena baada ya kiongozi wa kiraia kuondoa wanajeshi katika nafasi muhimu. Mwanajeshi shupavu, Kanali Assimi Goita alinusurika katika jaribio la kumuua lililotokea Julai 20 katika msikiti jijini Bamako.

Kanali huyo ameahidi kuirudisha nchi katika utawala wa kiraia kutokana na shinikizo la jumuiya ya kimataifa.
Nchini Sudan, utawala wa miaka 30 wa dikteta Omar al-Bashir ulifikia ukingoni wakati jeshi lilipochukua nchi Aprili 2019 baada ya maandamano kutamalaki kupinga kupanda kwa bei ya mkate.
Zaidi ya watu 250 walifariki katika maandamano hayo. Baadaye likaundwa baraza la mseto lililojumuisha wanajeshi na viongozi wa vyama vya kiraia Agosti 2019 na baadaye kuteuliwa waziri mkuu ambaye ni raia mwezi uliofuata.

Nchini Zimbabwe, Robert Mugabe, ambaye aliiongoza nchi kwa mkono wa chuma kwa miaka 37 tangu uhuru, alianguka mwaka 2017.
Aliondolewa na wanajeshi na wanachama wa chama chake cha ZANU-PF, ambao walimuweka makamu wa zamani wa rais, Emmerson Mnangagwa kushika nafasi yake.

Miaka miwili baadaye Mugabe alifariki akiwa Singapore akiwa na miaka 95.

Hali kama hiyo pia ilitokea nchini Misri, Burkina Faso na Guinea Bissau, ambako mapinduzi hayo ni ya nne tangu mwaka 1974 ilipopata uhuru kutoka kwa Wareno.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments