Michoro ya mwilini (tattoo) inavyoweza kukunyima fursa

Nilimsafirisha baba yangu Singapore, Ulaya na kwingineko kwa ajili ya kuokoa maisha yake, lakini ilishindikana akafariki dunia.

Kumbukumbu yake ndiyo nikachora tattoo mkono wa kulia ikiwa na maana ‘Mtoto wa baba’,” alisema Mwigizaji wa India, Priyanca Chopra alipofanya mahojiano na mtangazaji maarufu nchini Marekani, Opra Winfrey.

Priyanca ni mmoja kati ya wasanii wengi duniani wanaochora tattoo katika miili yao, wengine zikiwa na maana na wengine kwa ajili ya urembo.

Tattoo ya zamani kabisa kuwahi kuchorwa duniani ilipatikana katika maiti (mummy) ya mmoja wa mafarao wa huko Misri miaka 2000 kabla ya kuzaliwa Kristo. Hadi hivi leo maiti ambazo zimehifadhiwa kitaalamu nchini Misri zinaonyesha alama za michoro kwenye miili yao. Kwa mujibu wa wataalamu wa masuala ya historia ya Misri, tattoo kwa watu wa nchi hiyo zilikuwa na ishara ya ufufuo au uzima pamoja na uzazi/uwezo wa kushika mimba kwa wanawake.

Tatoo pcc

Hapa nchini watu maarufu na wasanii wameonekana kuchora tattoo katika miili yao, miongoni mwao wakiwemo Nasibu Abdul, Irene Uwoya, Shilole, Wema Sepetu, Jackline Wolper na wengine wengi.

Japo ni urembo uliodumu kwa miaka mingi, wataalamu wa afya wamekuwa wakikemea kuwa una madhara kiafya.

Mbali na kuhatarisha afya, pia mtindo huu wa urembo umewanyima baadhi ya watu fursa za kufanya shughuli fulani.

“Nilikuwa nina kila sifa ya kushiriki urembo, waandaaji pia walinifuata nianze ngazi ya kitongoji, nilikataa kwa kujua michoro ya miguuni na kifuani itaniangusha mbele ya safari kwa sababu haitakiwi,” anasema Sara Moses.

Kwa upande wa Rachel George, ambaye alikuwa akishiriki mashindano hayo ngazi ya wilaya jijini Dar es Salam, anasema:

“Ilibaki kidogo nitolewe lakini nikawahi kuifuta na kwa sababu haikuwa kubwa sana kovu halikuleta shida na rangi ya ngozi yangu nyeusi ilisaidia katika kuficha uangavu wa kovu lile.

“Nilikuwa naogopa kufuta kwa namna yoyote ile lakini nikakumbuka kuwa dawa ya nywele ikiwekwa kichwani huwa tunaungua, nikaamini inaweza kufuta, nikafanya hivyo na matokeo yakawa kama nilivyotarajia.

“Kiukweli ilinipa wakati mgumu, nilifikiria mazoezi yote niliyofanya, muda, pesa vyote ni sawa na kazi bure, sikutamani iwe hivyo bali kufuta ikawa chaguo sahihi”.

Rachel anasema japokuwa hakubahatika kushinda katika kinyang’anyiro hicho, lakini alitwaa taji la Miss Personality.

Siyo huko tu, bali zipo hata sehemu nyingine kama jeshini, lakini pia kuna kampuni mbalimbali zinazoendeshwa kwa imani za madhehebu ya dini huwa ni ngumu kutoa fursa za ajira kwa watu wenye michoro hiyo.

“Nililazimika kujichoma na pasi kidogo kidogo ili niifute tattoo, ilikuwa ya nge mdogo lakini ingeninyima fursa ya kuwa askari, sikufanikiwa kwa sababu nyingine, siyo mchoro maana niliufuta na kubaki na kovu,” anasema Emmanuel Silayo.

Silayo anasema akiwaona vijana wadogo wamechora miili yao anawahurumia sana kwa sababu anajua watajutia siku moja.

“Nikienda katika shughuli za familia nalazimika kuvaa nguo zitakazofunika mikono yangu kabisa, kwa sababu nimekuwa mtu mzima sifurahii kuonekana na michoro mwilini, hata wanaoniona hunishangaa, wanaoelewa ni wachache kuwa niliwahi kuishi nje ya nchi ambako kujichora ilikuwa fasheni,” anasema Mwanajuma Hijja, mwenye miaka 56.

Msanii kutoka kundi la TMK Wanaume family, Amani Temba ni miongoni mwa watu waliowahi kukumbwa na zahama ya kutotimiza ndoto ya kitu wanachokipenda kwa sababu ya tattoo.

Kwa mujibu wa simulizi za maisha yake, Temba alikuwa anapenda kuwa mwanajeshi na alifanya kila awezalo na kufanikiwa kujiunga na mafunzo hayo, lakini tattoo zikawa kikwazo cha kusonga mbele.

Huu ni ushahidi kwamba alikuwa akiipenda kazi hiyo kutoka moyoni, lakini kwa sababu ya tattoo aliyonayo ilikuwa ikimkwamisha, kwa maana hiyo hata iweje ndoto hiyo hatakuja kuitimiza.

Lakini watu waliochora tattoo hukosa pia fursa ya kuchangia damu hata ikiwa ni kwa dharura, hiyo ni kutokana na uwepo wa hatari ya kusambaza ugonjwa kwenda kwa mtu mwingine.

Daktari kutoka hospitali ya Anglikana Buguruni, John Nelson anasema watu wenye tattoo mara nyingi wanakataliwa kuchangia damu kwa sababu wengi huhusishwa na utumiaji wa vilevi pamoja na dawa.

Kitaalamu

Mbali na kuweka makovu yasiyofutika katika mwili, pia kwa mujibu wa Dk John Haule, uchoraji wa tattoo huweza kuleta magonjwa ya ngozi kwa wachoraji, ikiwemo vipele katika michoro yao, allergy (mzio).

“Pia unaweza kupata saratani, kwa sababu unapotoboa layer ya juu ya ngozi ya binadamu na kuweka wino wenye kemikali huweza kuleta madhara tofauti kati ya mtu mmoja na mwingine,” alisema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments