MIMBA ZA UTOTONI ZAWATESA BAADHI YA WASICHANA HANANG'

 BAADHI ya wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi miaka 17 Wilayani Hanang’ Mkoani Manyara, wameathirika kwa kupata mimba za utotoni kutokana na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi.


Kwenye baadhi ya maeneo ya Wilaya hiyo ikiwemo ya Kata ya Endasaki, baadhi ya wasichana wadogo wamekuwa wapata ujauzito ingali wakiwa wana umri mdogo.

Kutokana na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi kwao, wasichana hao wadogo ambao wana umri wa miaka 10 hadi miaka 17 wamekumbwa na tatizo hilo.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo ya watoto kupata watoto na kuitwa mama kabla ya muda muafaka inabidi elimu ya afya ya uzazi inapaswa kutolewa kwa wasichana hao wa eneo hilo.

Sheria ya mtoto inamtafsiri mtoto kama mtu mwenye umri chini ya miaka 18 na ana haki tano muhimu ambazo zinatambulika duniani kote.

Haki hizo za watoto ni haki ya kuishi, haki ya kuendelezwa, haki ya kulindwa, haki ya kushiriki na haki ya kutobaguliwa.

Kimsingi haki za mtoto huwa ni wajibu wa mtu mzima kutimiza mahitaji ya mtoto ili awe na afya, apate elimu na ashiriki katika kujenga nchi yake sasa na hasa atakapokuwa mtu mzima.

Sheria ya ulinzi na ustawi wa mtoto ya mwaka 2009 imelenga kuimarisha ulinzi, matunzo na haki za watoto

Msichana wa kata ya Endasaki, Aloycea John (16) siyo jina lake halisi anasema wasichana wengi wanakosa haki ya afya ya uzazi kutokana na elimu ndogo waliyonayo juu yao.

“Tatizo la wasichana wadogo wa umri wa miaka 10 hadi 17 kupata ujauzito kwenye eneo hili inapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa mstakabali wa maisha yajayo ya watoto hao wenye watoto,” amesema Aloycea.

Amesema Serikali inapaswa kuingilia kati suala hilo kwa ajili ya kutoa elimu ya afya ya uzazi kwa watoto wa eneo hilo ili kuondokana na changamoto hiyo iliyokithiri kwa baadhi ya wasichana hao wadogo.

Ofisa ustawi wa jamii wa wilaya ya Hanang’ Martha Sulle anasema kuwa wasichana wenye umri wa miaka 10 hadi 17 wa Wilaya ya Hanang’ wameathirika na mimba za utotoni kwa kipindi cha miezi 11 iliyopita.

Sulle anasema katika kipindi cha mwezi Julai 2020 hadi mwezi Juni 2021 mimba hizo za utotoni zilizoripotiwa ni mimba 183 hivyo wasichana 183 wamepata ujauzito sawa na mimba 16 kwa kila mwezi.

“Katika changamoto hiyo ya mimba za utotoni katika eneo hili wasichana 21 wenye miaka 13 hadi 15 walipata mimba na wasichana 162 wenye miaka 16 hadi 17 walipata mimba,” amesema Sulle.

Sulle anasema kuwa ofisi ya ustawi wa jamii ya halmashauri hiyo ilipata taarifa hizo za mimba kutoka vyanzo mbalimbali ikiwemo vituo vya afya, kwenye shule na dawati la polisi la jinsia.

Kwa upande wake, muuguzi msaidizi wa hosptali ya wilaya ya Hanang’ (Tumaini) Anasia Maliki akizungumza juu ya hilo amesema wasichana wana haki ya kuchagua watu wa kuolewa nao na siyo kuchaguliwa na wazazi wao.

“Wasichana na wanawake wanatakiwa kutambua kuwa wanapaswa kuilinda miili yao wenyewe na siyo kila mtu aichezee kwani ni kitu cha thamani,” anasema Maliki.

Amesema kwa bahati nzuri hakuna taarifa za msichana yeyote aliyepata maambukizi ya virusi vya ukimwi mara baada ya wao kufanya ngono zembe na kupatiwa mimba hizo.

Anasema wazazi na walezi wanatakiwa kuzungumza na wasichana wao kwani wakiwaacha bila kuwapa malezi bora wataendelea kubeba mimba zisizotarajiwa wakiwa bado wadogo.

Mkazi wa eneo hilo, Magreth Elias amesema wanajaribu kuhakikisha tatizo hilo linapatiwa ufumbuzi kwa jamii ya eneo hilo kukaa pamoja na kuzungumzia suala hilo ili lisiendelee kutokea.

“Ili kuhakikisha suala hilo linamalizika ni vyema ni bora kuhakikisha jamii ya eneo hili inakaa pamoja na kuzungumza juu ya hili na kumaliza tatizo hilo la mimba kwa watoto,” amesema Magreth.

Mmoja kati ya walimu wa shule ya msingi Endasak, James Bayo anasema elimu inapaswa kutolewa kwa wasichana hao wadogo na wazazi ili kuepusha changamoto ya watoto kupata mimba wakiwa wadogo.

Bayo anasema baadhi ya watoto hao waliolewa na kukatiza masomo yao kwani wasichana 20 waliripotiwa kupata ujauzito na kuacha masomo waliyokuwa wanaendelea nayo.

Anasema endapo elimu ya afya ya uzazi ikitolewa kwa wasichana hao wadogo juu ya tatizo hilo, wataelewa na kuepukana na tatizo hilo la mimba za utotoni lililopo kwa baadhi ya wasichana hao.

                                                     Na Joseph Lyimo, Hanang’

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments