MMOJA AFARIKI, 50 WANUSURIKA KIFO KWA KULA CHAKULA KINACHODAIWA KUWA NA SUMU KWENYE SHEREHE SINGIDA

Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge  akiwasalimia  na kuwapa pole manusura wa chakula  kinachosadikika kuwa na sumu.
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge  akiwasalimia  na kuwapa pole manusura wa chakula  kinachosadikika kuwa na sumu.


Na Edina Malekela,Singida
Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt. Binilith Mahenge amewatembelea wananchi waliolazwa katika Hospitali ya Mkoa huo baada kula chakula kinachosadikika kuwa na sumu ambapo katika tukio mtoto mmoja  mwenye umri wa miaka 7 amefariki dunia huku watu wengine 50 wakinusurika kifo.

Wakazi hao wa Kata ya Unyambwa kijiji cha Kisasida katika Manispaa ya Singida mkoani Singida walifikishwa hospitalini hapo jana baada ya hali zao kuwa mbaya kutokana na kula chakula kilichoandaliwa katika shughuli za ufunguzi wa Madrasa kijijini hapo.

Dkt. Mahenge amewapongeza madaktari wa Hospitali hiyo kwa jitihada za kuhakikisha wananusuru maisha ya wananchi hao ambapo kwa sasa hali zao zinaendelea vizuri na kuipongeza Serikali kwa kuweka miundombinu mizuri ya huduma katika sekta ya afya.

Ametoa wito kwa Viongozi wa Serikali na Dini kuwajibika kikamilifu katika kutoa elimu ya namna ya kuandaa chakula pamoja na kusimamia inapotokea sherehe mbalimbali kwenye maeneo yao ili kuepuka madhara ya namna hiyo.

Kwa mujibu wa Mganga mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa Banuba Deogratius amesema walipokea jumla ya wagonjwa 50,kati yao Wanawake 34 na Wanaume 16 ambapo hali zao zinaendelea vizuri na wanaanza kuwaruhusu baadhi yao kurudi nyumbani kuendelea na majukumu yao.

Aidha Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida Stella Mutabihirwa amesema wanawashikilia washukiwa 7 walioshiriki kuandaa chakula hicho kwa ajili ya uchunguzi na tayari wamechukua chakula hicho kwa uchunguzi zaidi.

Katika tukio hilo Kamanda amesema mtoto mmoja mwenye umri wa miaka (7) ambaye amefahamika kwa jina la Fahad Masudi amefariki dunia kabla ya kufikishwa hospitali kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments