Mo Dewji awaibukia kina Sakho mazoezini


Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi Simba, Mohammed Dewji ‘Mo Dewji’ ametinga katika mazoezi ya Simba jioni hii.

Simba walianza mazoezi saa 10:40 jioni na ilipofika saa 11:27 jioni aliwasili Mo Dewji akiwa katika msafara wenye magari matatu na pikipiki moja ya polisi.

Msafara huo wa Mo Dewji ulikuwa na pikipiki ya polisi iliyokuwa mbele kuongoza msafara baada ya hapo ikafuata gari nyingine, baada ya gari hiyo nyuma yake ndio ilikuwepo gari ya Mo Dewji aina Range Rover yenye rangi nyeusi kisha nyuma kulikuwa na gari nyingine waliyopanda walinzi wake wawili.

Mo Dewji baada ya kufika alishuka na kuanza kuwapungia mikono mashabiki waliokuwa uwanjani hapo ambao nao walilipuka kwa kupiga shangwe na kelele na kushangilia.

Bilionea huyo aliyekuwa na walinzi wake wawili nyuma alipomaliza kuwapungia mikono mashabiki alipokelewa na Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu ambaye alimpeleka mpaka sehemu ya kukaa.

Mo Dewji alikaa pamoja na Ofisa mtendaji mkuu, Barbara Gonzalez waliokuwa wakifuatilia mazoezi huku wakionekana kufanya mazungumzo na kuonyesha vidole uwanjani wakati wachezaji wakiendelea na mazoezi.

Ukiachana na Mo Dewji ambaye kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa uwanja wa Mo Simba Arena, kufika mazoezini kuangalia mazoezi ya Simba kulikuwepo na wadau wengine.

Miongoni mwa wadau hao alikuwepo aliyekuwa Makamo  rais wa Simba, Iddy Kajuna na Mjumbe wa bodi, Mohammed Nassor Kigoma.


MAZOEZI
Katika hatua nyingine kikosi cha Simba kiliendelea na mazoezi na walikazia katika maeneo matatu tofauti.

Eneo la kwanza Gomes, na wachezaji wake aliwapa mazoezi ya kucheza mpira na kuachia na kila mchezaji hakutakiwa kukaa na mpira au kugusa zaidi ya mara mbili.

Baada ya hapo wachezaji wa Simba, walipewa mazoezi ya kukaba na hakuna mchezaji ambaye alitakiwa kutembea pindi alipopoteza mpira.

Awamu ya mwisho ya mazoezi Gomes alichukua washambuliaji wake wote na kuwapa majukumu ya kufunga mabao kutokana na mashambulizi ambayo yatatengenezwa kutokea katikati ya uwanja au pembeni.

Kwenye mazoezi hayo Simba walimkosa winga wake, Bernard Morrison ambaye hata mechi na Yanga Jumamosi hatacheza kutokana na kufungiwa mechi tatu.

Winga Pater Banda hakufanya mazoezi pamoja na wenzake, kwani alitolewa na kuwekwa pembeni kufanya mazoezi mbalimbali ya nguvu na kujenga utimamu wake wa mwili ambayo yalikuwa yakisimamiwa na kocha wa viungo, Adel Zrane.

Imeandikwa na Thobias Sebastian, Oliver Albert, Ramadhani Elias na Leonard

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments