Recent-Post

Mwenyekiti TUGHE Taifa awapa tano wanawake kwa kurejesha uhai wa chama

 MWENYEKITI wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali Kuu na Afya (TUGHE) Taifa, Archie Mmtambo amesema wanawake ndio wamekisimamisha imara chama hicho kwani huko nyuma chama kilionekana kulegalega.

Kadhalika amewataka wafanyakazi kuacha kuogopa kujiunga na chama hicho, kwani lengo kuu la kuanzishwa kwa TUGHE ni kutetea maslahi ya wafanyakazi na si chama cha kiharakati kama ilivyo kuwa ikisemwa hapo awali.
Ameyasema hayo leo Septemba 28,2021 jijini hapa wakati akifungua Mkutano Mkuu wa uchaguzi wa wanawake TUGHE ambapo ameeleza kuwa lengo kuu la mkutano huo ni kufanya uchaguzi wa viongozi kwa nafasi mbalimbali wa chama hicho kwa upande wa wanawake.

"Mpaka kufikia hapa TUGHE imesimamishwa na wanawake,huko nyuma chama kiliyumba sana na yale maneno ya kwamba kujiunga na chama ni kama uanaharakati wa kupinga yale yanayosemwa na waajiri wetu, lakini tunawashuru kina mama hawa ndio waliosababisha chama hiki kusimama,"amesema Mmtambo.

Kwa upande wake Katibu wa TUGHE, Hery Mkunda ambaye amemaliza muda wake na anayewania nafasi hiyo kwa mara nyingine tena amesema mkutano huo unafanyika kila baada ya miaka mitano ambapo wanawake wa chama hicho uchagua viongozi wa nafasi mbalimbali.

"Leo ni uchaguzi wa TUGHE wanawake, lakini ikumbukwe kwamba katika katiba yetu ya TUGHE imeainisha kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu ikiwemo wanawake walemavu na vijana.

"Wanawake wamepewa kipaumbele zaidi kwani huko nyuma hawakuwa wakipata au kupewa nafasi sasa tumewaona wanawake na tunawapa nafasi ili waweze kujitegemea wenyewe na waimarishe chama," amesema Mkunda,

Hata hivyo TUGHE Taifa inatarajia kufanya uchaguzi wa viongozi hapo kesho Septemba 29, 2021 utakaojumuisha mwenyekiti Taifa, Katibu sambamba na wajumbe mbalimbali.
Na Doreen Aloyce,

Post a Comment

0 Comments