Recent-Post

Polisi, Magereza wadaiwa mabilioni Moshi

Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira mjini Moshi mkoani Kilimanjaro (Muwsa) inazidai taasisi za Serikali zilizoko chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani zaidi ya Sh3 bilioni hali inayoathiri  shughuli za uendeshaji wa mamlaka.

Taasisi hizo ni Jeshi la Polisi wanaodaiwa Sh1.6 bilioni, Chuo cha Polisi Moshi (CCP) Sh1 bilioni na Magereza Sh400 milioni.

Hayo yamebainishwa leo Jumatano Septemba 8, 2021 na kaimu mkurugenzi wa Muwsa, Kija Limbe wakati akitoa taarifa ya mamlaka kwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai alipofanya ziara ya katika mamlaka hiyo.

Limbe amesema mamlaka imeshindwa kukata maji kwa taasisi hizo kutokana na unyeti wake na kwamba suluhisho la kudhibiti deni hilo ni kufunga mita za malipo ya kabla ya matumizi.

Amesema katika kuzuia deni hilo kuendelea kukua, Muwsa tayari wamenunua mita za malipo ya kabla  443 ili kuzifunga kwenye taasisi hizo.

"Tunadai taasisi za umma zaidi ya Sh3 bilioni hii ni changamoto na si fedha kidogo, tungeipata leo, tungeweza kuboresha huduma kwenye maeneo ya pembezoni tunayoyahudumia ambayo Serikali inatamani yapate huduma sawasawa na ilivyo manispaa ya Moshi."

"Madeni haya yanatuathiri kwa kiasi kikubwa kwa sababu hatuwezi kuondoa huduma kwenye hizo taasisi kwa sababu ya unyeti wake na tumekuwa tukifanya ufuatiliaji wa karibu lakini tumekuwa tukipewa tu ahadi kwamba watalipa, " amesema.

Katika ufafanuzi zaidi ameeleza,  "lakini tunao mkakati wa kudhibiti madeni haya yasiendelee kukua, tayari tumenunua  mita 443 zipo stoo  ili kuhakikisha  taasisi hizi zinafungiwa mita hizo, kwa sasa tupo na mazungumzo nao ili kuweka mfumo wa kuwezesha kuzifunga na kila nyumba ijitegemee na mita yake."

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Dk Stephen Kagaigai amemuelekeza katibu tawala wa Mkoa huo, Dk Seif Shekalaghe kuwasiliana na wizara ambazo taasisi zake zinadaiwa ili kuona kama waliingiza deni hilo kwenye bajeti ya mwaka huu na kama hayakuingizwa yaingizwe bajeti ya mwaka ujao.

Mmeongelea deni ambalo mnalidai kwa taasisi za umma nakumbuka kuna maelekezo ya Serikali ya muda mrefu kwamba kwa madeni kama hayo yaingizwe kwenye bajeti za wizara husika."

Kwa hiyo Ras (katibu tawala mkoa) ningeomba ulichukue hilo, uwasiliane na taasisi za Serikali ambazo zinadaiwa kama hawakupanga kwenye bajeti hii, bajeti ya mwaka ujao  wazingatie wana deni na walipe na lengo ni kuwezesha mamlaka kuendelea kutoa huduma kwa ufanisi zaidi, " amesema Kagaigai.

Moshi.  bandolamedia.co.tz

Post a Comment

0 Comments