RAIS SAMIA AZINDUA MKAKATI WA UELIMISHAJI NA UHAMASISHAJI WA SENSA YA WATU NA MAKAZI 2022

SERIKALI imesema kupitia zoezi la Uhesabuji wa Sensa ya Watu na Makazi itawasaidia kufanya maamuzi ya rasilimali na namna gani ya kupeleka huduma za Kijamii na kimaendeleo ikiwemo Elimu, Afya, Miundombinu kulingana na idadi ya wananchi wa eneo husika.


Hayo yamesemwa na Rais Samia Suluhu Hassan leo jijini Dodoma wakati akizindua mkakati wa uelemishaji na uhamasishaji wa sensa ambayo itafanyika Agosti 2022 huku ikiwa na kauli mbiu inayosema "Sensa Kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa".

Rais Samia amesema ameupitia mkakati huo ambao unazinduliwa leo ambapo ameridhika nao huku akitaka wadau kutoka sekta mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini, vyombo vya habari, wasanii na wadau wa maendeleo kushirikiana na Serikali katika kuhamasisha zoezi hilo la sensa.

Amesema zoezi la sensa limekuepo kwa muda mrefu ambapo sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1910 ambapo Tanganyika ilikua chini ya Ujerumami huku sensa ya pili ya kisayansi ilifanyika mwaka 1967 baada ya Muungano wa Tanzania na Zanzibar na baada ya hapo imekua ilifanyika kila baada ya miaka 10 ambao ni utaratibu wa kimataifa.

Amesema lengo la sensa ni kufahamu idadi ya watu, mahali walipo, jinsia, umri, makazi na ubora wake, shughuli wanazofanya ambapo taarifa hizo zitasaidia kujua ongezeko la watu na hali ya uhamiaji huku akitolea mfano kutoka Vijijini kwenda Mjini na hata kutoka nje ya nchi.

 Bila kuwa na takwimu huwezi kushughulikia changamoto za ajira, kushughulikia matatizo ya watu wenye mahitaji maalum, kutoa huduma z kijamii wala kufanya maendeleo.

Kupitia taarifa za sensa huwezesha hata wawekezaji na wafanyabiashara kujua taarifa za eneo husika wanalotaka kwenda kuwekeza na kujua aina gani ya biashara inafaa wawekeze kulingana na eneo husika," Amesema Rais Samia.

Ameipongeza pia Kamati ya Taifa ya Sensa inayoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa kukamilisha mkakati huo wa uelemishaji na uhamasishaji wa sensa ambapo amesema wananchi wakipata elimu mapema juu ya zoezi hilo basi watajitokeza Kwa wingi kuhesabiwa.

Nitoe wito kutekeleza zoezi hili kwa gharama nafuu lakini kwa ufanisi mkubwa zaidi, wito wangu mwingine ni kutumia makundi mbalimbali kuhamasisha zoezi hili.

Niwaombe Viongozi wa Dini mnapotoa mahubiri kwa waumini wenu msisite kuwahamasisha kujitokeza kuhesabiwa, lakini pia Vyombo vya Habari kutenga muda wenu kwenye vipindi vyenu kuhamasisha zoezi hili bila kuwasahau wasanii na wanamuziki wetu," Amesema Rais Samia.

Kwa upande wake Makamu wa Rais Dk Philip Mpango ametoa wito kwa watanzania wote kujitokeza kuhesabiwa siku ya sensa Agosti 2022.

Baba wa Taifa alitufundisha ili tuendelee tunachohitaji zaidi ni Watu, Zoezi hili la Sensa linatuwezesha kujua Nguvu kazi yetu ili kupanga mipango yetu, Niwaombe kila mmoja wetu kujitokeza kuhesabiwa," Amesema Dk Mpango.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Sensa, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali inayoongozwa na Rais Samia imepanga kuinua uchumi wa viwanda na kumaliza changamoto ya ajira nchini lakini ili kutimiza malengo hayo ni lazima kuwepo na takwimu sahihi ambazo zinapatikana kwenye taarifa za Sensa.

" Mhe Rais naomba nikuhakikishie kuwa kazi hii ambayo umetupatia ya Sensa ya Sita tutaisimamia ipasavyo na kwa weledi wa hali ya juu, nikuhakikishie watu wote watakaolala nchini usiku wa kuamkia siku ya sensa Agosti 2022 wote watahesabiwa," Amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Rais Samia Suluhu Hassan leo jijini Dodoma wakati akizindua mkakati wa uelemishaji na uhamasishaji wa sensa ambayo itafanyika Agosti 2022 huku ikiwa na kauli mbiu inayosema "Sensa Kwa Maendeleo, Jiandae Kuhesabiwa".

                                                  Charles James


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments