Recent-Post

Refarii atoboa siri ya kumuonya mara sita bondia msauzi aliyemchapa Tony Rashid

Licha ya kuonywa mara sita na refarii, hiyohaikumpunguza kasi, Bongani Wonder Boy Mahlangu kuondoka na ubingwa wa Afrika (ABU) aliouchukua mikononi mwa Mtanzania, Tony Rashid usiku wa kuamkia leo kwenye pambano la utangulizi kusindikiza lile la Hassan Mwakinyo na Julius Indongo.

Mahlangu raia wa Afrika Kusini ambaye jina lake la utani ni Dancing Shoes aliwaduwaza wengi alipotwaa taji hilo ugenini kwa kumchapa kwa Technical Knock Out (TKO)raundi ya 12 na ya mwisho ya pambano, mwenyeji aliyekuwa akiutetea ubingwa huo wa uzani wa super bantam.

Ubingwa huo umemrejesha upya kwenye renki bondia huyo wa Afrika Kusini ambaye hakuwa 'active' tangu Desemba 12, 2019 alipocheza pambano lake la mwisho na kuchapwa kwa pointi na Patrick Kinigamazi huko Cirque de Noel, Geneva pambano la ubingwa wa dunia wa WBF.

Jana bondia huyo alirejea tena ulingoni, licha ya tofauti ya umri aliokuwa nao dhidi ya mpinzani wake, alitumia mbinu ya kutembea muda wote ulingoni na kushambulia kwa kushtukiza tangu raundi ya kwanza hadi ya 11 huku katika raundi hizo, refarii wa pambano, Chaurembo Palasa akimuonya mara sita, jambo ambalo baadhi ya mashabiki ukumbini hapo walililamikia na wengine kuamini refa huyo alitaka 'kumbeba' Mtanzania.

"Nilikuwa nikimuonya aache kukimbia kimbia, asimame na kucheza ngumi kwani ile haikuwa marathoni, haiwezekani bondia muda wote anakimbia kimbia tu ulingoni, hivyo mara zote nilipokuwa nikimuonya ilikuwa ni kumtaka asimame apigane," anasema Palasa.

Hata hivyo mbinu za bondia huyo zilimsaidia raundi y 12, alipomshambulia Tony Rashid hadi akalewa kabla ya kuokolewa na mwamuzi baada ya kurushiwa ngumi nyingi mfululizo bila majibu, lakini kabla ya mshidi kutangazwa kukaibuka sintofahamu ulingoni huku kambi ya Tony ikimtuhumu mpinzani wao kucheza mchezo mchafu.

"Kuna vitu wasaidizi wake wa ulingo walikuwa wakimpa ambavyo inasemekana ni vya kuongeza nguvu, lakini pia kwenye glovu zake kuna vitu aliweka aliporudi raundi ya 12," Tony aliiambia Mwananchi Digital mara baada ya kushuka ulingoni.

Alisema mpizani wake alichukuliwa sampo ya damu na mkojo kwenda kupimwa kama kweli kuna kitu alitumia na anasubiri majibu baada ya ripoti ya madaktari.

Hata hivyo Palasa, refarii wa pambano hilo anasema hakuna ukweli juu ya madai hayo, yalitokea baada ya karatasi kuonekan ulingoni, ikadaiwa imetoka kwenye glovu ya 'Msauzi' huyo, ingawa hakuna uthibitisho.

"Kambi ya Tony ndiyo ilidai hivyo, lakini hakuna uthibitisho na mpinzani wake amepewa mkanda wa ubingwa," alisema Palasa aliyewahi pia kuwa bondia na kubainisha ambacho kimemponza Mtanzania huyo hadi kupoteza taji hilo kuwa ni nidhamu ya mchezo.

"Tony  amejichelewesha mwenyewe kumaliza pambano, aliporudi kwenye raundi ya 12, aliona tayari ameshinda, wakati muda ulikuwa bado, mpinzani wake katumia uzoefu na kumaliza pambano hilo," amesema.

Post a Comment

0 Comments