Recent-Post

Ronaldo ampiga marufuku mama yake kutazama mechi

 


Manchester, England. Mshambuliaji mpya wa timu ya Manchester United, Cristiano Ronaldo amefichua kuwa amemkataza mama yake mzazi, Maria Dolores dos Santos Aveiro kuangalia mechi kubwa ambazo atakuwa uwanjani anacheza kutokana na matatizo ya kiafya yanayomsumbua.

Inaelezwa kuwa Maria amewahi kuanguka na kuzimia mara mbili katika mechi ambazo alikuwa jukwaani akimtazama Ronaldo akicheza.

Tatizo kubwa ambalo linaelezwa kumsumbua mama wa nyota huyo ni hisia kali alizonazo kwa mwanaye ambaye alipata shida kumlea mpaka akaweza kufikia ndoto za kuwa mchezaji mkubwa duniani.

Taarifa ambazo amenukuliwa Ronaldo akizitoa ni kwamba, kuna wakati mama yake alianguka na kuzimia uwanjani na kama haitoshi aling’oka mpaka meno.

Hali hiyo imemfanya Ronaldo kuwa mkali kwa mama yake kutokana na majanga anayoyapata kutokana na kutazama michezo mikubwa ambayo kwa sasa anashindwa kuvumilia kumuona Ronaldo akicheza.

Ronaldo alisema hajui kwa nini siku hizi mama yake amekuwa akishindwa kuzishinda hisia zake wakati anaangalia mechi ambazo yupo uwanjani, kiasi cha kumfanya apoteze fahamu na amekuwa akimuweka wazi kuwa hana baba ambaye alifariki dunia tangu akiwa mdogo na kwa sasa hayupo tayari kukubali mama yake pia apoteze kutokana na vitu vya kawaida.

Licha ya Maria kuwa na mchango mkubwa kwenye maisha ya soka ya Ronaldo, lakini kinara huyo wa upachikaji mabao wa muda wote katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya ameamua kumkataza mama yake kutazama michezo mikubwa akiwa uwanjani kama vile robo fainali, nusu fainali na hata fainali akihofia kupata tena matatizo ya kuanguka.

Taarifa zinaeleza kwamba tayari Ronaldo amemtafutia mama yake watu watakaokuwa wanamfariji akiwa nyumbani wakati akiwa uwanjani akicheza, ikiwa ni kwa ajili ya kujali uhai wa mzazi huyo ambaye kwa sasa anakabiliwa na tatizo hilo akiwa na umri wa miaka 66 na ndiye nguzo pekee ya familia.

Mchezaji huyo alirejea England katika timu iliyompandisha chati ya Manchester United akitokea Juventus ya Italia, baada ya kuichezea kwa misimu mitatu.

Post a Comment

0 Comments