Serikali yawataka wachimbaji madini kuacha kutumia njia asili

Serikali imewataka wachimbaji wa madini walioko Kanda ya Ziwa kutumia huduma za utafiti ushauri elekezi na uchambuzi wa sampuli katika maabara ili kuchimba kwa tija badala ya kutumia njia za asili ambazo hazina tija na zinasababisha hasara.

Hayo yamesemwa leo Jumanne septemba 21, 2021 na Waziri wa Madini, Doto Biteko wakati wa hafla fupi ya kufungua kituo cha taasisi ya Jiolojia na utafiti wa madini (GST) mkoani Geita kitakachohudumia wachimbaji kutoka mikoa ya kanda ya ziwa

Biteko amesema utafutaji wa madini ni sayansi hivyo wachimbaji hawana budi kutumia sayansi kutafuta madini  na kuwataka kutumia wataalam wa GST  waliosomeshwa na Serikali kufanya tafiti kwenye maeneo yao na kuachana na uchimbaji wa kubahatisha usio na tija .

Akizungumzia kufunguliwa kwa kituo hicho Biteko amesema sio tuu kitasaidia wachimbaji kuchimba kwa tija bali pia itaongeza mapato kutoka Sh400 milioni zinazokusanywa na GST kwa sasa hadi kufikia Shilingi bilioni moja.

Amesema awali wachimbaji walilazimika kusafirisha sampuli za mchanga hadi Dodoma lakini sasa uwepo wa kituo hicho utawezesha wachimbaji kupata taarifa sahihi za maeneo yao kabla ya kuanza uchimbaji.

Kwa mujibu wa Waziri Biteko Serikali inakusudia kujenga jengo la madini  mkoani Geita litakalogharimu Sh4.5 bilioni lengo likiwa ni kusogeza huduma zote muhimu kwa wachimbaji .

Katibu mkuu wa Wizara ya Madini, Simon Msanjila amesema kwa sasa sekta ya madini inachangia asilimia sita kwenye pato la taifa na kuwa lengo ni kuchangia kwa asilimia 10 ambapo kwa mwaka huu wa fedha wizara hiyo inakusudia kukusanya Sh650 bilioni.

Amesema moja ya kazi itakayofanywa na kituo cha GST ni pamoja na kutoa mafunzo kwa wachimbaji wadogo kama vile namna ya uchukuaji sampuli  ili kuchimba kwa tija,kutoa ushauri elekezi kwa wadau wa sekta ya madini ,kufanya utafiti wa kina wa jiyosayansi ili kubaini maeneo mapya yenye viashiria vyua uwepo wa madini.

                   Geita. By Rehema Matowo


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments