Recent-Post

SIMBA SC YAJA NA TAMADUNI ZA TIMU KUBWA DUNIANI


KAMA zinavyofanya timu nyingine duniani, Klabu ya Simba kwa kushirikiana na Wadhamini wake, MeTL imezindua moja ya tamaduni zinazofanywa na Klabu hizo katika kusherehesha mashabiki wake, kuwapa hamasa na kuleta umoja katika Soka hususani kuanzia msimu ujao wa mashindano wakianza na Simba Day, 19 Septemba 2021.

Simba SC imezindua Karagosi (Mascot) waliopewa jina la MO Rafiki, ambao watatumika kusherehesha Mashabiki wake pindi timu hiyo inapokuwa Uwanjani katika michezo yake mbalimbali sambamba na kampeni zake za kutoa misaada kwa makundi maalum.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu hiyo, Barbara Gonzalez amesema ujio na ubunifu wa ‘Mascot’ hao lengo kubwa kugusa maisha ya watu, kuleta furaha kila sehemu timu inapokuwa ikicheza na hata kwenye kampeni zake mbalimbali.

Barbara amesema, “Tunaona timu zilizoendelea ulimwenguni, timu za Arsenal, Manchester United, Everton na nyingine, zinafanya ubunifu kama huu ili kuleta hamasa, umoja kwa mashabiki na hata kwa Wachezaji wanakuwa na furaha wakiwaona ‘Mascot’ hao.

Nakumbuka Mesut Özil alijitolea kumlipa Mascot wa timu ya Arsenal baada ya kutangazwa hali ya ukata kipindi cha Corona. Tunaona umuhimu wa Mascot hadi Wachezaji walitaka aimsiondoke ndani ya Klabu”, ameeleza Barbara.

Simba SC inajiandaa na tamasha lake la Simba Day, Septemba 19, 2021 ambapo itacheza mchezo wa kirafiki na Kabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Tamasha hilo litaenda sambamba na utambulisho wa Kikosi chake cha msimu wa 2021-2022.
                                     Na Bakari Madjeshi.

Post a Comment

0 Comments