SIMBA wamepania kufanya funika katika tamasha lao la Simba Day Septemba 19 kwa kucheza na timu iliyotwaa ubingwa wa Afrika zaidi ya mara mbili. Mwanaspoti linajua kwamba Simba ina timu nne mkononi. Tp Mazembe ya Demokrasia ya Congo, Al Ahly ya Misri, El Merrikh ya Sudan na Mamelody Sundowns ya Sauzi.
Licha ya kwamba wanafanya siri kubwa lakini Mwanaspoti linajua kwamba wameipa kipaumbele zaidi Mamelody ambao ni wapinzani wa Kaizer.
Simba Day tamasha ambalo ufanyika kila mwaka, linatarajiwa kupigwa katika uwanja wa Benjamini Mkapa Dar es Salaam huku sapraizi kibao zikiandaliwa katika tamasha hilo.
“Al Ahly wanaratiba ya Super Cup ambao mchezo wao utachezwa Septemba 25 nchini Qatar sasa hawa kuwapata kuna ugumu kidogo,”alidokeza mmoja wa viongozi wa Simba huku akiongeza kuwa wanahitaji kucheza na timu ambayo itawapa upinzani wachezaji wao na wanasimba kupata burudani.
“Mpaka sasa hakuna timu ambayo tumekubaliana nayo kutokana na ratiba za timu nyingi kuwa finyu lakini Simba Day ni jambo la Kitaifa, na matukio yake yanafanywa kikubwa,” alisema Mtoa habari huyo.
Hata hivyo, habari zinasema kuwa Simba inaangalia pia gharama za kuisafirisha timu kuja na kulala hivyo hawahitaji papara katika hilo kwa kuwa jukumu hilo ni lao na wamepania kuhakikisha siku hiyo inakuwa ya aina yake.
0 Comments