Recent-Post

Simba yapania kimataifa

MRATIBU wa Simba, Abbas Ally amesema maandalizi yanayoendelea Karatu mkoani Arusha yanatoa picha halisi jinsi kikosi hicho kitakavyofanya vizuri kwenye michuano mbalimbali.

“Wachezaji wote wana ari kubwa tangu tumefika hapa, hili kwetu kama viongozi tunalichukulia kama mafanikio makubwa kwa sababu lengo letu ni kuendelea kutawala soka la Tanzania,” alisema.

Aliongeza, wachezaji waliopo timu ya taifa wanapaswa kurejea haraka iwezekanavyo ili kujiunga na wenzao kwa ajili ya maandalizi.

“Wachezaji waliopo timu ya taifa hawatopewa mapumziko, tupo nje ya muda hivyo kocha wetu Gomes amewataka wakimaliza majukumu yao kwenye timu za taifa warejee kambini mara moja,” alisema.

Kuhusu michezo ya kirafiki Abbas alisema wapo kwenye mchakato wa kutafuta mechi mbili au tatu za kirafiki ili kutoa fursa nyingine kwa wachezaji kutengeneza muunganiko hasa kwa wale wapya.

“Tumekuwa na maombi kwa timu kadhaa zikihitaji kucheza na sisi, Namungo ni miongoni mwao lakini zipo timu kutoka Burundi, Kenya na zinginezo lakini uamuzi wa mwisho tutaufanya kwa siku za hivi karibuni kujua tutacheza na timu zipi,” alisema.

Akizungumzia wapinzani wao TP Mazembe ambao watacheza nao kwenye kilele cha “Simba Day’, Abbas alisema wamechagua timu bora Afrika ambayo itawapa kipimo sahihi kuhusu timu yao.

“Hakuna asiyewajua TP Mazembe ubora wao hivyo viongozi wa juu wameona ni vyema kucheza nao siku hiyo ili vijana wetu waendelee kupata uzoefu,” alisema.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa ni Februari 2, mwaka huu na timu hizo zilitoka sare ya 0-0, katika kombe maalumu lililoandaliwa na klabu ya Simba likifahamika kama Simba Super Cup.

Kikosi hicho kwa sasa kimeweka kambi Karatu Jijini Arusha kikijiandaa na msimu ujao baada ya ile ya awali nchini Morocco.

Post a Comment

0 Comments