Recent-Post

SIO ZENGWE: Sakata la Manara linafikirisha mageuzi yetu


NI bahati mbaya sana kwamba macho ya wengi wiki iliyopita yalielekezwa katika kuangalia kama Kilele cha “Wiki ya Wananchi” kitafunika au la, hasa wakiangalia ushiriki wa Haji Manara, ambaye amevuka mto kutoka Simba na kutua Yanga.

Mafanikio ya maadhimisho hayo hayakuhusishwa moja kwa moja na waandaaji, bali na usajili huo wa mchezaji wa nje ya uwanja na utakuwa uthibitisho kuwa ndiye alikuwa siri ya mafanikio ya upande aliotoka.

Ile safari ndefu ya mabadiliko ya kimfumo katika muundo na uendeshaji wa klabu ya Yanga, itawekwa kando kwa sasa hadi hapo kutakapoonekana kuna chokochoko ndipo itaibuliwa tena.

Hali ni kama hiyo upande wa Simba, ambako wanapambana kwa nguvu zote kuonyesha kuwa mkuu wa wa zamani wa kitengo cha habari hakuwa muhimu kwa jinsi anavyojaribu kujieleza.

Zaidi ya yote wanafanya kila jambo kutaka kuonyesha kuwa ile safari ya mabadiliko iliyoanza miaka minne iliyopita, inaendelea vizuri na kwa namna yoyote ile haiwezi kuathiriwa na kuondoka kwa mtu mmoja tu; tena ambaye alikuwa muajiriwa.

Pande hizo zote mbili zinafanya jitihada kubwa ili mashabiki na wanachama wao waone kuwa kilichofanyika—kumuachia Haji aondoke au kumchukua Haji ili awe msemaji mpya—ulikuwa ni uamuzi sahihi na mambo yanaendelea kama yalivyopangwa.

Lakini pamoja na yote, sakata hilo la Haji Manara linafikirisha, hasa kwa safari hiyo ya mageuzi ambayo pande zote zinaendelea nayo.

Katika kuonyesha kuwa wako makini, Yanga wameeleza kuwa wameandaa adidu za rejea za kazi ya Manara ili kuepusha mgongano wa majukumu na wafanyakazi wenzake. Hii inatokana na ukweli kwamba tayari Yanga ina mkuu wa habari wa klabu, yaani Bumbuli, huku ikiwa imeshaachana na Antonio Nugaz, aliyekuwa ofisa uhamasishaji, uhusiano na mashabiki.

Kwa huko alikotokea, Haji alikuwa akitekeleza majukumu hayo yote, yaani kuhamasisha na kutoa habari za Simba na sasa anapewa majukumu ambayo yanaweza kufinyisha uwanja wake wa kujidai.

Kama nilivyoandika huko nyuma, kuondoka kwa Haji Simba kulifichua mambo mengi ya kimfumo, ambayo awali hayakuweza kuonekana iwapo asingeondoka. Inawezekana kuwa hakuwa na adidu za rejea za majukumu yake na hivyo alikuwa akifanya chochote alichoona kwa maoni yake kuwa ni sahihi.

Kwa kuamini hayio, sishangai napomuona Haji akimshambulia Mwekezaji wa Simba, Mohammed Dewji, ambaye kimadaraka alikuwa juu sana, kiasi kwamba hata kupata nafasi ya kuongea na ofisa habari ilitakiwa iwe kazi ngumu.

Kama Mwenyekiti wa Bodi na mwekezaji anaweza kumuita Mkuu wa Kitengo cha Habari, ambaye anaajiriwa na anawajibika kwa Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Simba, kwa nini Haji asijione kuwa alifikia daraja la kiongozi na si muajiriwa?

Kwa hiyo mazingira ya kazi na kutokuwepo kwa mfumo wa kueleweka wa uwajibikaji, mipaka ya kazi na muundo thabiti unaoheshimika, ndiko kulikomfanya, Haji aonekane na pengine ahisi kuwa nafasi ya mkuu wa kitengo cha habari ilikuwa kubwa sana na hivyo hakuna ambaye angeweza kumzuia.

Hali kama hiyo inaonekana kuanza kujijenga Yanga, licha ya kusema kuwa imemuandalia adidu za rejea za majukumu yake ili kuepusha mgongano.

Mara baada ya kutambulishwa, Haji alitangaza kuwa siku iliyofuata wangezindua jezi za msimu huu. Bila shaka taarifa hiyo ilitakiwa kutolewa na Ofisa Habari na si mhamasishaji, ingawa siku hiyo angehusika sana kwa kuwa ilihusisha mashabiki na wanachama kufahamu na kuzijua jezi mpya na muhimu zaidi, kuzinunua.

Hilo ni jambo dogo tu kwa kuchambua siku za mwanzo za Haji Yanga zinazoonyesha safari ya mabadiliko haijakaa sawa. Hapa hoja kinzani inaweza kutolewa kirahisi tu kuwa; “mabadiliko bado hayajakamilika”.

Lakini jingine la kujiuliza kuhusu mabadiliko yanayoenda kufanyika, hivi nafasi aliyopewa, Haji ipo kwenye muundo ambao Yanga wanaanza kuufuata? Au ilikuwa muhimu kumpata, Haji kwanza halafu baadaye kumtafutia majukumu na mwisho kumtengenezea adidu za rejea za majukumu yake?

Ni muhimu sana kuzingatia kila jambo wakati wa kufanya mabadiliko ya kimuundo na kimfumo kwa kuwa madoa machache yanaweza kuchukuliwa kuwa hoja nzito kwa watu walio makini na hivyo kuwachukulia kuwa wapinzani na mwisho kuvuruga safari.

Sakata la Haji Manara linatakiwa litumike kutufikirisha kama tuko katika njia sahihi ya mabadiliko au tunayaimba kinywaji, lakini matendo ni tofauti na hali halisi.

Post a Comment

0 Comments