Taliban wamerudi madarakani kama walivyoondoka - 16

Kampeni ya kupingana na dini iliyofanywa na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Afghanistan (DRA) na baadaye na Warusi ilitengeneza mazingira ambayo yaliviwezesha vikundi vya itikadi kali za kidini vya Afghanistan kunufaika.

Kuibuka kwa washabiki wa imani kali nchini Afghanistan hakujatokana na jamii na utamaduni wa nchi hiyo, bali msimamo mkali ulioingizwa nchini na vikundi vya kigeni, hasa wakati wa uvamizi wa Urusi, ambavyo vilinufaika na mapambano dhidi ya Warusi na baadaye wakaendelea kunufaika na machafuko ndani ya Afghanistan.

Kwa karne nyingi, Afghanistan iliathiriwa na mafundisho ya viongozi mbalimbali wa imani ya Sufi katika dini ya Kiisilamu kama Khajah Abdullah Anssari, Mawlana-e-Balkhi, Naser Khosrow, Al-Bironi, Khoshhal Khan Khatak, Hamid Baba na kadhalika.

Soma hapa: Taliban wazidisha mashambulizi-13

Viongozi hawa walihimiza amani, uvumilivu na upendo. Waliamini kwamba mwanadamu anaweza kuingia katika eneo la ukweli usio na mwisho, ambapo ufalme wa Mungu uko, ikiwa anaweza kufikia kiwango cha juu kabisa cha upendo kwa Mungu.

Ushawishi wa mafundisho ya kisiri na ya kisufi katika malezi ya kitamaduni ya Afghanistan yalisaidia jamii za huko kudumisha mila zilizokuwako kabla ya Uislamu kama sherehe ya mwaka mpya na wazo la Pushtonwali (njia ya maisha ya Pashtun ambayo inategemea ukarimu, heshima na kulipiza kisasi).

Pashtun ni kundi au ukoo unaotawala nchini Afghanistan ambalo limepigana kwa nguvu kutunza ukuu wao katika historia ya Afghanistan.

Matokeo ya muundo huu wa kitamaduni ni kwamba vikundi tofauti vya dini, kama vile Wayahudi, Wahindu na Sikh, wameishi na Waislamu wengi kwa umoja.

Maendeleo haya ya kihistoria ya kijamii na kitamaduni baadaye yaliwekwa katika katiba ya Afghanistan, ambayo ilitoa haki sawa kwa raia wake wote bila kujali asili yao ya kabila na dini.

Soma hapaKuondoka na kurudi kwa kundi la Taliban

Mgawanyo wa Serikali na dini ulikuwa sehemu muhimu ya siasa za kitaifa nchini Afghanistan. Kihistoria, Afghanistan haikuwahi kutawaliwa na viongozi wa dini, na viongozi wa serikali walikuwa wakisimamia shughuli za umma kila wakati na taasisi za kidini zilisimamiwa kwa uhuru au chini ya usimamizi wa serikali.

Katika matukio mengi, mamlaka za Serikali zilikuwa na uhusiano mzuri na imani na taasisi za kidini zilimuunga mkono kiongozi wa serikali kitaifa.

Mwanzoni mwa miaka ya 1970, Serikali ya Afghanistan iliwapeleka wanafunzi kupata elimu ya juu Mashariki ya kati, hususan katika nchi ya Misri.

Baadhi ya wanafunzi hawa waliathiriwa na itikadi ya kisiasa ya wale walioitwa ‘Muslim Brotherhood’ wa Misri, ambacho ni moja ya vikundi vya awali vya Kiisilamu.

Miongoni mwa wahitimu hawa wa Afghanistan walikuwa Burhanadin Rabbani, Abdul Rabe Rassul Sayyaf na Sibqatollah Mujaddadi, ambao walikuja kuanzisha Muslim Brotherhood wa Afghanistan waliojulikana kama Ikhwan-al-Muslimun (IM).

Hawa, na wengine kadhaa, walikuja kuwa viongozi muhimu katika harakati za Mujahidina. Zaidi ya yote, Hekmatyar na Rabbani walichukua siasa kali kuelekea serikali na jamii.

Baada ya njama iliyoshindwa dhidi ya utawala wa Rais Mohammad Daud Khan mwaka 1974, viongozi hao wa IM walikimbilia Pakistan na kupata msaada kutoka kwa Serikali ya Pakistan chini ya utawala wa Zulfaghar Ali Bhutto.

Katika mwaka uliofuata, jeshi la IM lilivuka mpaka kwenda Afghanistan ili kuondoa uasi dhidi ya utawala wa Daud, lakini lilizuiwa na vikosi vya serikali vikisaidiwa na jamii za wenyeji.

Soma hapa: Asili ya uadui wa Taliban na Marekani-2

Kwa viongozi mashabiki wa Afghanistan, kutumia dini kwa faida yao ya kisiasa na kuondoa kabisa wapinzani wao ilikuwa njia ya kawaida ya kufanya siasa. Kutokana na hili, idadi kubwa ya wanasiasa mashuhuri wa Afghanistan, wasomi na makamanda wa Mujahideen huko Afghanistan waliuawa wakati na baada ya majeshi ya Urusi kuondoka.

Mauaji haya yalifanywa na wanamgambo wa Hezb-e-Islamic Hekmatyar na chama cha Jamaiat-e-Islami Rabbani, chini ya uangalizi wa Shirika la Kijasusi la Pakistan (ISI) huko Pakistan na wakati mwingine kwa ushirikiano wa majasusi wa Urusi ndani ya Afghanistan.

Vita vya siri na kampeni ya ugaidi na vikundi vya washabiki wa Kiislamu vya Afghanistan nchini humo na Pakistan vililazimisha idadi kubwa ya wanasiasa wa Afghanistan kukimbilia uhamishoni Ulaya na Amerika Kaskazini.

Kuundwa kwa Dola ya Ufalme wa Kiislamu Afghanistan (IEA) mwaka 1996 kulifanyika kama matokeo ya ombwe la uongozi lililosababishwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyoanza mwaka 1992.

Taliban, kwa msaada wa moja kwa moja wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Pakistan iliyoongozwa na Jenerali Babar, ilifaidika na ile hali ya kukosekana kwa uongozi wa kitaifa nchini Afghanistan na kuleta asilimia 80 ya nchi chini ya udhibiti wao.

Lakini baada ya hapo, zile ahadi za Taliban za amani na haki zilipotea, zikibadilishwa na sera zao kali na ukatili dhidi ya wapinzani wao wa kisiasa na dhidi ya wale ambao si wapinzani wao, lakini wana siasa za wastani.

Ubaguzi wao wa kijinsia na wa kikabila, wa kidini, ukiukaji wa haki za kimataifa za binadamu na uharibifu wa urithi wa kihistoria, ulimvuruga karibu kila mtu katika jamii za watu wa Afghanistan katika maeneo yanayodhibitiwa na Taliban.

Ingawa waliondolewa madarakani mwishoni mwa mwaka 2001 baada ya uvamizi wa kijeshi wa Marekani mara baada ya Septemba 11, miaka 20 baadaye wamerejea tena madarakani kama walivyoingia.

                                               By William Shao

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments