Wachezaji 28 Yanga watakaoshiriki kimataifa hawa hapa

 


YANGA ipo kambini ikiendelea kujipanga na mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya awali wakikutana na Rivers United ya Nigeria na uhakika pale makao makuu ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) upande wa Idara ya Mashindano yamefika majina 28 tu, huku ikielezwa watani wao ina watu 31.

Yanga hawakutaka msafara mrefu kama ambavyo kanuni zinawapa nafasi wakitakiwa kusajili wachezaji 40 kwa mashindano hayo ambapo wao wakawasilisha kikosi chao kamili kilichosajiliwa msimu huu pekee.

Orodha ya uhakika ambayo Mwanaspoti imeipata ni kwamba jina la mwisho kukamilishwa katika usajili huo ni kiungo Khalid Aucho ambaye Waarabu wa Lel Makkasa inayoshiriki Ligi Kuu Misri walikuwa wanadengua kutoa uhamisho wake wa kimataifa lakini baadaye wakaachia wenyewe.

Orodha ambayo Yanga imewasilisha inawajumuisha makipa 3 ambao ni Diarra Djigui, Erick Johola na Ramadhan Kabwili huku mabeki wakiwa 9 ambao ni Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Yannick Bangala, Dickson Job, Bakari Mwammnyeto.

Wengine ni Kibwana Shomari, Djuma Shaban, David Bryson, Adeyun Saleh na Paul Godfrey ‘Boxer’ watakaosimamia uimara wa Yanga katika safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Yanga imewajumuisha viungo 6 ambao Mukoko Tonombe, Aucho, Feisal Salum, Zawadi Mauya, Deus Kaseke, Jesus Muloko, Farid Mussa, huku kwenye eneo la ushambuliaji itakuwa na watu 6 ambao ni Fiston Mayele, Heritier Makambo, Yacouba Songne, Said Ntibazonkiza, Yusuf Athuman na Heritier Makambo.

Hata hivyo, Yanga itakuwa na nafasi 12 za kuongeza mastaa wengine endapo itafanikiwa kutinga hatua ya makundi ya ligi hiyo baada ya kushindwa kutumia nafasi hiyo katika usajili wa sasa.

Yanga itacheza mechi ya kwanza dhidi ya Rivers, Septemba 12 kwenye Uwanja wa Mkapa na marudio yao yatafanyika wiki moja baadaye nchini Nigeria na kama vijana wa Jangwani wakipenya hapo inaweza kukutana na mshindi kati ya Fasil Kenema ya Ethiopia na Al Hilal ya Sudan.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments