WACHIMBAJI WADOGO WALIA KUKOSA MIKOPO, BENKI ZAJIBU

Shirikisho la vyama vya wachimbaji nchini (Femata) limeziomba taasisi za fedha kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo kwa vitendo ili uchimbaji uwe na tija kwao na Serikali kwa ujumla.

Hayo yamesemwa na Rais wa Femata, John Bina wakati wa hafla ya ufunguzi wa maonyesho ya nne ya teknolojia ya dhahabu yaliyofunguliwa leo septemba 22, 2021 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mkoani hapa.

Amesema benki zimekua zikidai kuwakopesha wachimbaji wadogo lakini hawatekelezi kwa vitendo na kuiomba serikali kutoa ruzuku ya vifaa ili waweze kuchimba kwa tija.

Amesema kama serikali itaweka nguvu kwenye sekta ya uchimbaji itawezesha kuwa na uchimbaji bora na wenye tija.

Bina amesema kwa mwaka wa fedha uliopita wachimbaji wadogo wamechangia Sh 180bilioni kwenye mapato ya Wizara ya madini na endapo watashikwa mkono kwa kupatiwa mkopo wataweza kuchangia zaidi kwenye pato la Taifa.

Akijibu malalamiko hayo, Meneja biashara wa benki ya CRDB Kanda ya Mangharibi, Jumanne Wagana amesema changamoto kubwa ni wachimbaji kuchimba bila kuwa na utafiti wa kijiolojia hivyo kuzifanya taasisi za fedha kuogopa kuwakopesha.

Amesema ni sawa na kuwekeza kwenye kamari na kuwa bado wanaendelea na tafiti kuona ni namna gani ya kuwasaidia wachimbaji wadogo ambalo ndio kundi kubwa kwa kanda ya ziwa.

Kwa upande wake mkurugenzi wa biashara wa benki ya biashara (NBC), Elvis Ndunguru amesema benki hiyo inaendelea kutoa mafunzo ya elimu ya biashara kwa wachimbaji wadogo ili waweze kuwapatia mikopo.

             By REHEMA MATOWO

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments