WANAHABARI WASHAURIWA KUJIUNGA NA CHAMA CHA WAFANYAKAZI WANAHABARI (JOWUTA)

 WANAHABARI Nchini wameshauriwa kujiunga na Chama cha Wafanyakazi Wanahabari Tanzania (JOWUTA,) ili kuwa na sehemu maalumu ya kusemea changamoto zao pamoja na kupigania maslahi, stahiki muhimu na haki zao za msingi.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo maalumu ya kitaifa kwa waandishi wa habari vijana mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Wanahabari Tanzania (JOWUTA,) Claud  Gwandu amesema JOWUTA kwa kushirikiana na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi duniani,  'International Federation of Journalist' (IFJ)  wameandaa mafunzo hayo ya siku mbili kwa waandishi wa habari vijana ambao wengi wamehitimu masomo yao na kuajiriwa ili kuweza kuwaandaa kuwa viongozi wa chama hicho na kuwashauri kutumia fursa ya kujiunga katika chama hicho kitakacholinda maslahi yao.

Amesema, vijana wanajukumu kubwa la kuendeleza chama hicho hasa katika wakati huu ambao dunia ipo katika mabadiliko makubwa ya teknolojia na fursa lukuki kupitia mageuzi hayo hivyo ni vyema wakajiunga katika umoja huo ambao ni sehemu sahihi ya kusemea changamoto zao.

Gwandu amesema, katika semina hiyo mada mbalimbali ikiwemo mazingira ya kazi kwa waandishi wa habari vijana, haki zao za msingi, unyanyasaji wa kingono mahali pa kazi, masuala ya TEHAMA  pamoja na mazingira ya ufanyaji kazi wakati  huu wa ugonjwa wa COVID-19 na umuhimu wa kuwa mwanachama wa JOWUTA zitajadiliwa kwa msaada wa wataalam mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi.

Pia ameishukuru serikali kwa kukitambua chama hicho na kukishirikisha katika shughuli mbalimbali pamoja na Baraza la Habari Tanzania (MCT,) ambalo limekuwa msaada mkubwa kabla na baada ya kuanzishwa kwa umoja huo.

Akimwakilisha mtendaji mkuu wa MCT, Meneja  Rasilimali Watu na Utawala wa baraza hilo Ziada Kilobo amesema, JOWUTA ni chama muhimu sana kwa wanahabari na MCT ikiwa taasisi ya kihabari itaendelea kushirikiana na vyama hivyo katika kuhakikisha wanahabari wananufaika kupitia vyama vyao hasa JOWUTA ambayo ni muhimu katika kutetea maslahi yao.

Ameeleza kuwa tangu kusajiliwa kwake JOWUTA ina wanachama 350 kutoka mikoa 15 na kuwashauri wanahabari wengi zaidi wakiwemo vijana kujiunga na chama hicho kinachosimamia maslahi ya wafanyakazi na kukikuza  kupitia ada za uanachama.

Akitoa salamu kutoka Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi duniani,  'International Federation of Journalist' (IFJ)  Mkurugenzi wa IFJ, Afrika Pa Louis Thomasi kutoka Dakar, Senegal amesema, wanahabari barani humo bado wanasita kujiunga na umoja huo na hukumbuka umuhimu wake wanapopatwa na majanga hasa ya maslahi ya kazi na kuwashauri waandishi vijana kujiunga na umoja huo na kuwashauri viongozi kuendelea kushirikiana na Serikali na Wizara husika katika kusimamia maslahi bora ya wafanyakazi wanahabari.



Meneja Rasilimali Watu na Utawala kutoka Baraza la Habari Tanzania (MCT,) Ziada Kilobo akizungumza na waandishi wa habari wakati wa mafunzo hayo na kuwataka kuwa mabalozi kwa wanahari kote nchini ili waweze kujiunga na chama hicho, leo jijini Dar es Salaam.
Mjadala ukiendelea.
mwenyekiti wa Chama cha Wafanyakazi Wanahabari Tanzania (JOWUTA,) Claud  Gwandu (katikati,) akizungumza wakati wa mafunzo hayo na kuwashauri wanahabari vijana kujiunga na umoja huo ili waweze kuwa viongozi bora wa JOWUTA, leo jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa IFJ, Afrika Pa Louis Thomasi kutoka Dakar, Senegal akitoa mada wakati wa mafunzo hayo.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments