Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) nchini Tanzania imetoa vitambulisho vya uraia milioni 9.4 tangu ianze kuzalisha vitambulisho hivyo huku vitambulisho milioni 1.3 vikiwa havijachukuliwa.
Hayo yamesemwa leo Jumamosi Septemba 4, 2021 na msemaji mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa wakati akizungumza na Watanzania kupitia vyombo vya habari.
Amesema shughuli hiyo inaendelea vizuri ambapo hivi sasa vitambulisho vya Taifa milioni 9.4 vimetolewa na kati ya hivyo vitambulisho milioni 8.5 vimeshahakikiwa.
“Uhakiki unaangalia kitambulisho kimoja kimoja, unaangalia kama jina limekaa sawa na taarifa zote zilizopo kwenye kitambulisho,”amesema.
Amesema Watanzania milioni 7.2 wamechukua vitambulisho vyao huku milioni 1.3 vikiwa bado katika ofisini walizoombea.
“Mkachukue vitambulisho vyenu mlipokwenda kujisajili. Vipo baadhi vilikuja katika ofisi lakini walivibadilisha kwa sababu walitoa taarifa visivyo, hawa mchakato wa kubadilisha unachukua muda lazima mamlaka ijiridhishe isije ikawa ni nia ovu ama anachukua taarifa za mtu mwimwingine,” amesema.
0 Comments