Recent-Post

WATUMISHI WATATU WA AFYA WAKAMATWA KWA WIZI WA MASHINE YA OKSIJENI SIMIYU

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamshina Msaidizi wa Polisi Richard Abwao akiongea na waandishi wa Habari (hawapo pichani), ofisini kwake.

Mfano wa Mashine ya kuangalia Mapigo ya Moyo, Upumuaji, Wingi wa hewa ya Oksijeni katika damu kwa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji (Cadiac Monitoring Accessories), kwa hisani ya Mtandao.

Na Costantine Mathias - Simiyu.
JESHI la Polisi Mkoani Simiyu linawashikilia watumishi watatu wa Idara ya Afya kwa wizi wa Mashine ya kuangalia Mapigo ya Moyo, Upumuaji, Wingi wa hewa ya Oksijeni katika damu kwa mgonjwa aliyefanyiwa upasuaji ambapo mashine hiyo iliibiwa ikiwa ndani ya chumba cha upasuaji mkubwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Simiyu (Nyaumata).

Katika taarifa iliyolewa leo kwa waandishi wa Habari na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Kamishna Msaidizi wa Polisi Richard Abwao imeeleza kuwa uchunguzi katika eneo la tukio (Hospitali) ulibaini kuwa chumba hicho cha upasuaji hakikuvunjwa.

Mnamo tarehe 20/09/2021 majira ya saa 07:30 asubuhi huko Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Simiyu (Nyaumata), iliyopo mtaa wa Nyaumata, Wilaya ya Bariadi, Mkoa wa Simiyu, Getrude Emmanuel (45), msukuma, mkristo na katibu wa hospitali ya mkoa Simiyu, aligundua kuibiwa kwa mashine 01 inayojulikana kwa jina la Cadiac Monitor Accessories yenye namba za usajili ex-7c051585 yenye thamani ya tsh .7,820,000/= iliyokuwa kwenye chumba cha kufanyia upasuaji wa macho’’ amesema Kamanda Abwao.

Amefafanua kuwa "Kiini cha tukio hili ni kujipatia kipato kisicho halali, wafanyakazi katika chumba hicho cha upasuaji wamekamatwa na wanahojiwa kuhusiana na tukio hili ni Paul Igosha (37), msukuma, mkazi wa Somanda, Neema Msekile (24), mnyakyusa, mkazi wa Kidinda na Edward Yirika (27), muha, mkazi wa somanda ambao wote ni wauguzi katika chumba cha upasuaji wa macho hospitali ya nyaumata’’.

Kamanda Abwao ameeleza kuwa baada ya tukio hilo kuripotiwa kituoni hapo upelelezi mkali ulianza mara moja kwa kukagua eneo la tukio na kuhoji baadhi ya mashahidi na baada ya mahojiano hayo timu hiyo ya makachero waliwakamata watumishi wa chumba cha upasuaji wa hospatali hiyo ambao ni Paul Igosha, Neema Msekile na Edward Yirika ambao walihojiwa lakini walikana kuhusika na tukio hilo.

Ameendelea kuwaambia Waandishi wa Habari kuwa (jana) tarehe 22/09/2021 majira ya saa 09:0hrs alikamatwa Allen Cosmas (30), Daktari wa usingizi, chumba cha upasuaji ambaye pia alihojiwa na makachero na hatimaye kukiri kuhusika na tukio hilo, ambapo alieleza kuwa mashine hiyo ameuza mkoani Mwanza .

Ameongeza kuwa timu hiyo ya makachero ilielekea Mkoani Mwanza eneo la kona ya Bwiru wilaya ya Ilemela, Mkoani Mwanza na kufanikiwa kumkamata rafiki wa Daktari huyo aitwaye Enord Iginatio Kalekezi (29), Daktari kituo cha afya Kisorya wilayani Bunda Mkaoni Mara, ambaye alihojiwa na kueleza kuwa ameuza kwa Daktari aitwaye David Omollo (32),  Daktari wa hospitali binafsi iitwayo Royal Hosptal iliyopo kona ya Bwiru wilaya ya mkoa wa Mwanza.

Amesema timu ya makachero ilifika hospitalini hapo na kufanikiwa kuikamata mashine hiyo iliyokuwa kwenye chumba cha upasuaji hospitalini hapo (Royal Hospital) na tayari imeshaletwa na imeifadhiwa kituo cha polisi Bariadi kama kielelezo.

Akaongeza kuwa mpaka sasa watuhumiwa watatu ambao ni Allen Cosmas, David Omollo na Edward Ignatio wapo mahabusu kituo cha polisi bariadi kwa mahojiano na baada ya mahojiano kukamilika watafikisha mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.

Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dk. Mike Mabimbi amedhibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku akidai kuwa wizi huo umetokea usiku wa kuamkia Jumapili (Sept 19, 2021) wiki iliyopita, na kwamba jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

DK. Mabimbi ameongeza kuwa licha ya mashine hiyo kuibiwa huduma kwa wagonjwa hazijasimama kwa kuwa hospitali hiyo ilikuwa na mashine tatu za kwa ajili ya utaoji wa huduma kwa wagonjwa, pia ameongeza kuwa washatoa taarifa Wizara ya Afya, Jeshi la Polisi pamoja na Ofisi wa Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu.

Post a Comment

0 Comments