WAWAKILISHI KIMATAIFA KAZI BADO IPO


 KAZI inaendelea kwa sasa hasa kwa timu ambazo zinaiwakilisha Tanzania kwenye mashindano ya kimataifa.

Tunazo timu nne na hii ni fursa kubwa ambayo inabidi ilindwe na kila timu kwa sasa ili na wakati ujao tupeleke timu nne pia kwani ni heshima na furaha kwa Tanzania kuwa na timu nyingi ambazo zinaipeperusha bendera.

Ukianza kwenye Kombe la Shirikisho kuna Azam FC na Biashara United hizi zote zimeanza kwa ushindi kwenye mechi zao za awali.

Ni Azam FC hawa walikuwa nyumbani pale Uwanja wa Azam Complex na waliibuka na ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Horseed FC ya Somalia na Biashara United hawa Wanajeshi wa mpakani wao kazi yao ilikuwa dhidi ya FC Dikhil ya Djibouti.



Ushindi wa bao 1-0 ugenini bado haimaanishi kwamba kazi imekwisha ukurasa bado unaendelea kufunguka na muhimu kwa kila mchezaji kujua kwamba kazi ipo palepale.

Mchezo wa pili ni zaidi ya fainali kwa kuwa mwisho zinahukumu nani ataendelea mbele na nani atapewa mkono wa shukrani aendelee na maisha mengine katika hatua ya awali.

Ipo wazi kwamba wawakilishi wetu kwenye Kombe la Shirikisho mnastahili pongezi lakini hamstahili kujisahau kwa kuwa kazi bado ipo kuweza kusaka ushindi kwenye mechi za marudio.

Ukiwatazama Azam FC watakuwa nyumbani kwa mara nyingine licha ya kwamba ule mchezo wa awali uliochezwa Azam Complex wao walikuwa ni wenyeji.



Ikumbukwe kwamba mchezo wa pili nao utakuwa na ushindani kama ilivyo kwa wenyeji namna wanavyosaka ushindi. Kwenye mchezo wa kwanza kipindi cha kwanza Azam FC iliweza kutoshana nguvu na Horseed hivyo inapaswa kuongeza umakini katika mchezo wa pili.

Biashara wanajukumu la kuongeza juhudi kwenye mchezo wao wa marudiano pia ili kuweza kulinda ushindi ambao mlipata awali.

Ukiweka kando na hawa wanaowakilisha nchi kwenye Kombe la Shirikisho, Yanga na Simba hawa wapo kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

Yanga imeanza kwa kuchechemea mchezo wa awali baada ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Rivers United na kazi haijaisha.

Mchezo wa pili ni muhimu kwa Yanga kufanya maboresho kwa yale ambayo waliyafanya mchezo wa awali, inawezekana kama wageni waliweza kushinda hapa Tanzania basi na Yanga inawezekana kushinda Nigeria.

Kikubwa ni maandalizi na kila mmoja kuweza kutimiza majukumu yake kwa wakati. Kwenye mpira kila kitu kinawezekana kikubwa ni maandalizi mazuri na nidhamu katika utendaji wa kazi.

Simba hawa hawataanza hatua ya awali kwa kuwa waliweza kufanya vizuri msimu uliopita baada ya kutinga hatua ya robo fainali.

Kwa hatua ambayo waliifikia msimu uliopita hapa wanakazi nyingine ya kufanya ili kuweza kupata ushindi kwenye mechi watakazocheza ili waweze kufika mbali zaidi.

Haitakuwa kazi rahisi kuweza kupenya kwenye nafasi ambayo walifika msimu uliopita ikiwa kila kitu watachukulia kawaida kwani ni muhimu kusaka ushindi kwenye kila hatua.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments