Yanga hii nje moto, ndani balaa

WACHEZAJI wanne waliokuwa katika kikosi cha Yanga msimu uliopita, ndio watakaotazamwa msimu ujao kama wataweza kuingia katika kikosi cha kwanza cha timu hiyo baada ya mabadiliko makubwa yaliyofanyika.
Wapo waliojihakikishia nafasi ya kuendelea kuanza kwenye kikosi cha kwanza na ni viungo wawili Faisal Salum na Mukoko Tonombe pamoja na mabeki, mmoja kati ya Bakari Mwamnyeto na Dickson Job pamoja na Kibwana Shomary.
Pia wapo wapya watakaopewa nafasi kubwa ya kuanza kwenye mashindano yote na kutokana na mabadiliko hayo Mwanaspoti limefanya uchambuzi wa kutosha kulingana na mifumo mitatu ya (4-2-3-1, 4-4-2 na 4-3-3), na Kocha wa Yanga, Nesreddine Nabi ambaye anapenda kuitumia mara kwa mara.

MAKIPA

Msimu uliopita alikuwepo Metacha Mnata aliyedaka kwenye mechi nyingi akisaidia na Mkenya Faroukh Shikhalo na msimu huu wote wawili hawapo kwenye kikosi hicho.

mapema pic 1

Msimu huu Yanga imeleta makipa wengine wawili, Djigui Diarra atakayekuwa chaguo la kwanza kutokana na ubora wake aliouonyesha akiwa na kikosi cha timu ya Taifa ya Mali na klabu aliyotoka ya Stade Malien pamoja na mchezo wa kirafiki dhidi ya Zanaco.
Ramadhani Kabwili aliyekuwepo msimu uliopita na mwingine mpya, Erick Johora watachuana nafasi ya kipa chaguo la pili atakayekaa benchi.

MABEKI WA KULIA
Msimu uliopita, Kibwana Shomary alionyesha kiwango safi kwenye nafasi hii na msimu huu Yanga imemwongeza, Djuma Shabani kuongeza ushindani katika eneo hilo.
Hapa kuna vita kubwa na atakayeonyesha kiwango mazoezini ndiye atapewa nafasi ya kuanza.
Hata hivyo, huenda wakaanza wote kwenye nafasi ya beki wa kulia na kushoto kama ilivyokuwa katika mechi dhidi ya Zanaco.
Hii inampa wakati mgumu beki Paul Godfrey ‘Boxer’ ambaye msimu uliopita hakupata nafasi kuwaweka benchi Kibwana na Djuma wanaotazamwa kama chaguo la kwanza.

MABEKI WA KUSHOTO

Katika eneo la kushoto hapa Nabi atakuwa na machaguo mawili kwanza kumtumia kati ya watatu waliokuwepo sasa, Yassin Mustapha, Adeyun Saleh na David Bryson ambaye amesajiliwa msimu huu.
Mushapha bado anauguza majeraha yake ya msimu uliopita kwani kati ya Adeyun na Bryson mmoja wapo anaweza kucheza, lakini kuna chaguo la pili kutokana na ubora wa mabeki wa kulia, Kibwana anaweza kucheza katika nafasi hii.
Kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Zanacco kutokana na ubora wa mabeki hao wa pembeni, Nabi alimpanga Djuma kulia na Kibwana kushoto na kuwacha mabeki hao wote wa kushoto nje.

MABEKI WA KATI

Usajili wa Yannic Bangala utakuwa na faida kwa Yanga kwani Mkongomani huyo anaweza kucheza nafasi ya beki wa kati kama ilivyokuwa FAR Rabat ya Morocco klabu ambayo ametokea au kiungo mkabaji kama ilivyokuwa katika mechi ya Zanaco.
Kutokana na umahiri wake huo wa kucheza zaidi ya nafasi moja maana yake, Bangala anaweza kupangua ukuta wa Yanga na kati ya Bakari Mwamnyeto na Dickson Job waliotumika zaidi msimu uliopita mmoja wapo atampisha.
Abdallah Shaibu ‘Ninja’ kutokana na kusuasua kupata nafasi ya kucheza msimu uliopita katika kikosi cha kwanza mara kwa mara na usajili huo ambao Yanga wamefanya maana yake anaweza kuendelea kusota benchi.

VIUNGO WAKABAJI

Ukiachana na Bangala ambaye anaweza kucheza katika nafasi ya kiungo mkabaji kwenye eneo hilo ushindani utaendelea kuwepo kama msimu uliopita kati ya Mukoko Tonombe na Zawadi Mauya.
Awali Mukoko ndio alikuwa akitumika zaidi lakini msimu ulipo changanya Mauya nae alikuwa akipewa nafasi katika kikosi cha kwanza kutokana na ubora wak alikuwa akitumika pamoja na Tonombe.
Ni wazi kutokana na maingizo mapya ya Bangala na Khalid Aucho kati ya Mukoko na Mauya kuna mmoja wapo atakwenda benchi ili kumuacha mwenzake akicheza zaidi katika kikosi cha kwanza.

VIUNGO WASHAMBULIAJI

Miongoni mwa eneo lingine ambalo litakuwa na ushindani zaidi msimu ujao katika kikosi cha Yanga ni safu ya viungo wanne washambuliaji ambao watakuwa wakionekana zaidi kiwanjani.
Kutokana na ubora wa Feisal Salum kila anapopata nafasi ya kucheza ataendelea kudumu kwenye kikosi cha kwanza kama ilivyo kwa Aucho ambaye anatazamwa kuingia katika nafasi hiyo kama atakuwa bora.

mapema pic 2


Upande wa viungo kutokea pembeni Juses Moloko ndio anatazamwa kama mbadala wa Tuisila Kisinda aliyeuzwa Morocco na wingi mwingine kati ya Dickson Ambundo, Deus Kaseke, Farid Mussa na Ditram Nchimbi kati yao ataanza upande mwingine.
Balama Mapinduzi kutokana na kukaa nje kwa muda mrefu kutokana na kuuguza majeraha yake atakuwa na kazi kubwa ya kuonyesha ubora kama aliokuwa nao kabla ya kuumia ili kupata nafasi ya kucheza.

WASHAMBULIAJI

Nabi mara nyingi hupenda kuanza na straika mmoja asilia kama ilivyokuwa katika mechi ya Zanacco kutokana na ubora aliokuwa nao, Heritier Makambo na rekodi aliyoweka awali anapewa nafasi ya kuanza.

Ukweli usiopingika Makambo ni kipenzi cha kila ambaye anaipenda Yanga kutokana na uwezo wake wa kufunga mabao aina mbalimbali, kukaa na mpira, kuwasumbua mabeki, kutoa pasi za mwisho na sifa nyinginezo.
Fiston Mayele ndio anaonekana kuwa mbadala wa Makambo au katika mechi nyingine Nabi anaweza akaanza nao wote wawili na akapunguza kiungo mmoja mshambuliaji ambaye atakuwa kati au pembeni.
Mfungaji bora wa msimu uliopita, Yacoub Sogne aliyemaliza msimu na mabao nane anatakiwa kuwa bora na imara zaidi wa kutimiza majukumu yake kila anapopewa nafasi ya kucheza kwa wakati huu anaonekana kuwa mabadala wa hao wawili.
Usajili mpya, Yusuph Athumani nae anatakiwa kucheza katika kiwango bora kwa maana ya kufunga mabao katika kila nafasi ambayo atapata, kuisaidia timu kupata matokeo mazuri pamoja na mambo mengine kwani akishindwa kufanya hivyo anaweza kuishia benchi kama mechi iliyopita dhidi ya Zanaco.

 

Post a Comment

0 Comments