Recent-Post

Yanga yaichapa Pan African, Mayele aendelea kutupiaYanga imeendelea kupata mechi za kirafiki na jioni hii imefanikiwa kupata ushindi mwembamba dhidi ya Pan African.

Bao la kipindi cha kwanza la mshambuliaji Fiston Mayele limetosha kuihakikishia Yanga ushindi huo katika mchezo wao wa pili wa kujipima nguvu tangu wakutane na Zanaco ya Zambia katika kilele cha wiki ya mwananchi ambapo Yanga ililala kwa mabao 2-1.

Mayele alifunga bao hilo kwa ufundi akimnyanyulia kipa wa Pan aliyetoka kuja kuzuia shambulizi hilo lililotokana na mpira mrefu wa beki wa Yanga.

Bao hilo la Mayele linakuwa la pili katika mechi ya pili mfululizo akitangulia kufunga bao moja wakati Yanga ikishinda mabao 3-1 dhidi ya Friends Ranger.
Mshambuliaji Heritier Makambo hakuwa na bahati ya kufunga baada ya kuingia kipindi cha pili kufuatia kupoteza nafasi ya wazi shuti lake likigonga mwamba.

Yanga bado inaendelea kucheza mechi za kirafiki sambamba na mazoezi kwa lengo la kujiweka tayari kabla ya kukutana na Rivers United ya Nigeria katika mchezo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hizo zitakutana Septemba 12 katika Uwanja wa Mkapa kabla ya kurudiana wiki moja mbele nchini Nigeria.

Post a Comment

0 Comments