Recent-Post

Yanga yashtaki FIFA, yathibitisha kuwakosa watatu

Uongozi wa Yanga umethibitisha kuwakosa wachezaji wao watatu kuelekea mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United.

Msemaji wa Yanga, Haji Manara amesema  kwamba Yanga itawakosa wachezaji watatu ambao ni kiungo Khalid Aucho, beki Djuma Shaban na mshambuliaji Fiston Mayele.

Soma zaidi: GSM akomaa ishu ya kina Mayele, Djuma

Gazeti la Mwanaspoti limekuwa gazeti la kwanza kutoa habari ya wachezaji hao kuzuiwa na Shirikisho la Soka Afrika CAF katika toleo lake la leo Jumatano Septemba 8, 2021

Manara amesema kukosekana kwa wachezaji hao hakuna makosa yoyote ya klabu yao ambapo matatizo hayo yamesababishwa na makosa ya klabu walizotokea kushindwa kuachia hati za uhamisho (ITC).

Soma zaidi:CAF yazuia watatu Yanga, yumo Djuma na Aucho

"Yanga ilifanya kila kitu kwa wakati katika kuomba hati za uhamisho mchezaji kama Khalid Aucho alikuwa na mgogoro na klabu yake hawakumlipa mishahara yake na Fifa wakamvunjia mkataba na kuwa mchezaji huru," amesema Manara.

"Djuma Shaban naye tuliomba vitu vyote kwa wakati lakini klabu yake wakatoa ITC siku moja baada ya dirisha kufungwa hapo Yanga inakosa gani.

Aidha Manara ameongeza kwamba kutokana na changamoto hizo tayari uongozi wa klabu yao wamewasiliana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF ) kuwaomba Fifa kuingilia kati hatua hiyo.

Tunaamini wenzetu wa Fifa watatupa majibu mazuri lakini hata hivyo Yanga imejiandaa vizuri na kikosi ni kipana wapo wachezaji hata wakikosekana hao wapo ambao wataziba nafasi zao."


Post a Comment

0 Comments