Recent-Post

BIASHARA UNITED MARA YASHINDWA KUSAFIRI LIBYA

KLABU ya Soka ya Biashara United Mara imeshindwa kusafiri kuelekea nchini Libya kutokana na kukosekana kwa vibali vya anga vya Kimataifa nchini Sudan, Sudan Kusini na kibali cha kutua Benghazi, Libya ambapo mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Al Ahly Tripoli SC utachezwa.

Taarifa iliyotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) imeeleza kuwa licha ya kupatikana Ndege ya kukodi kutoka ATCL safari hiyo itashindikana na Shirikisho limeiandikia barua Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuhusiana na dharura hiyo iliyojitokeza wakati timu hiyo ya Tanzania ikijiandaa kusafiri kuelekea nchini Libya.

TFF imeeleza kuwa imewaomba CAF kusogeza mchezo huo wa mkondo wa pili hadi Jumanne ya Oktoba 27, 2021 ili kupata vibali hivyo vya kusafiri hadi Libya. Imeelezwa kuwa kumekuwa na changamoto ya upatikanaji wa vibali katika Mamlaka za Anga katika nchi za Sudan, Sudan Kusini na Libya siku za Ijumaa na Jumamosi.

“Ili kutumia anga la nchi nyingine ni lazima kupatikana vibali maalum kwa nchi husika hiyo ni kutokana na sababu za kiusalama, TFF na Wizara ya Michezo zinaendelea na jitihada kupata vibali hivyo vya anga”, imeeleza Taarifa ya TFF.

Biashara United Mara walitarajiwa kucheza kesho Jumamosi Oktoba 23, 2021 ikiwa ni mchezo wa mkondo wa pili dhidi ya Al Ahly Tripoli ambapo mchezo wa mkondo wa kwanza Biashara United waliibuka na ushindi wa bao 2-0 katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, Tanzania.

Na Mwandishi Wetu

Post a Comment

0 Comments