BIASHARA UNITED YATAMBA MBELE AL AHLY

 

Mshambuliaji wa Biashara United FC, Atupele Green akijaribu kumtoka Mchezaji wa Al Ahly Tripoli ya Libya katika mtanange uliopigwa jioni ya leo kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, ambapo Biashara waliibuka na ushindi wa bao 2-0 kwa mabao ya Deogratius Judika Mafie na Atupele Green.

KLABU ya Biashara United ya Musoma mkoani Mara nchini Tanzania imeonyesha ubabe mbele ya timu kongwe ya Al Ahly Tripoli SC ya Libya kwa kupata ushindi wa bao 2-0 katika mchezo uliopigwa jioni ya Oktoba 15, 2021 kwenye dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Mabao ya Biashara United katika mchezo huo yalifungwa na Mshambuliaji Deogratius Judika Mafie dakika ya 39 na bao la pili limefungwa na Mshambuliaji Atupele Green kipindi cha pili kwenye dakika ya 61 ya mchezo huo ambao Biashara walitamba kwa kiasi kikubwa kutokana na kuwepo nyumbani (Home Advantage).

Mchezo wa marudiano utachezwa kati ya Oktoba 22-23, 2021 nchini Libya, hivyo Biashara United wanatakiwa kulinda ushindi huo kutokana na ubora wa Wachezaji wa timu hiyo yenye mataji 12 ya Ligi Kuu nchini humo na wenye Wachezaji wengi waliosheheni kwenye timu ya taifa ya Libya

Katika hatua nyingine, wawakilishi wengine kwenye Michuano hiyo, Azam FC watacheza na Klabu ya Pyramids ya Misri katika uwanja wao wa Azam Complex, Chamazi Dar es Salaam siku ya Jumamosi Oktoba 16, 2021.

Biashara walifuzu hatua ya kwanza kucheza na Al Ahly Tripoli SC ya Libya baada ya kuwasukuma nje ya Michuano hiyo, FC Dhikil ya Djibouti kwa jumla ya mabao 3-0 katika michezo miwili, iliyopigwa nchini Djibouti na Tanzania.

Azam FC wamefuzu hatua hiyo kucheza na Pyramids FC baada ya kuwasukuma nje ya Michuano hiyo ya Kombe la Shirikisho, Klabu ya Horseed FC ya Somalia kwa jumla ya mabao 4-1 katika michezo yote iliyopigwa nchini Tanzania.

Na Bakari Madjeshi, 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments