CCM yaweka msimamo kwa watumishi


Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeonya kuwa hakitamfumbia macho mtumishi yeyote wakiwemo wa umma ambaye utendaji kazi wake utakuwa kero kwa wananchi.

Pia, kimesema kitaendelea kuwa daraja la kuwafikishia huduma bora Watanzania ili kuchochea kasi ya maendeleo nchini.

Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka ameyasema hayo leo Oktoba 24, 2021 wakati akizungumza na mamia ya vijana walioshiriki kongamano la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha kupatikana kwa mkopo wa masharti nafuu wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).


" CCM tunawataka watumishi wote wa umma nchini kuendeleza utendaji kazi wenye weledi, nidhamu na heshima kwa wananchi kwani hao ndio waajiri wa Serikali iliyopo madarakani,” amesema Shaka.


Amesema Rais Samia na Serikali yake wanaamini katika uthubutu, uzalendo na ni waumini wa nidhamu ya kazi na matokeo yenye kuchochea ustawi wa wananchi.

Amesema kuna tabia inayoanza kujitokeza kwa baadhi ya watumishi wa umma kuzembea katika kitimiza majukumu yao na kufanya kazi wa mazoea bila ya kuheshimu wala kuwajali wananchi.

“Siri ya Chama Cha Mapinduzi kuendelea kuaminiwa na Watanzania ni kwa sababu kinabeba agenda za maendeleo, kinatoa matumaini na suluhu kwa changamoto zinazoikabili jamii. Hatutarajii kuwa tutakuwa kimya kwa wachache wenye malengo tofauti na yale ya kuwatumikia Watanzania ambayo ndio mambo ya msingi,” amesema Shaka.

Pia, Shaka amempongeza Rais Samia kwa kusimamia kikamilifu sera zake za maendeleo na shirikishi katika kuongoza nchi tangu ameingia madarakani.

Amesema dhamira njema ya Rais Samia ni kuona Watanzania wanaendelea kupata huduma bora huku akisisitiza uwazi katika masuala yote ya maendeleo.

" Rais Samia amekuwa muwazi kwa mambo yote yanyohusu maendeleo. Tumepata fedha za mkopo ameelekeza kila wizara kuweka mchanganuo na kueleza kila hatua ya utekelezaji.

Ametuambia katika miezi sita yake madarakani nini amefanya na wote tunaona kile alichokieleza kwa macho huku kwenye maeneo yetu,” amesema Shaka, ambaye amewahi kuwa Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana (UVCCM) na baadaye Katibu wa CCM Mkoa Morogoro.

Awali, Katibu wa UVCCM Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Kilakala, amesema vijana wapo pamoja na Rais Samia na wataendelea kuwa mstari wa mbele katika utekelezaji wa maagizo na maelekezo mbalimbali yanayotolewa ili kuendelea kujenga Tanzania bora

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments