Chadema yapingana na Jaji Siyani uamuzi kesi ya Mbowe

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema hakiridhishwi na uamuzi uliotolewa na Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa kuwa umekiuka masuala ya msingi ya sheria.

Hatua hiyo imetokana na mahakama hiyo kutupilia mbali mapingamizi katika kesi ya ugaidi inayomkabili Mbowe na wenzake watatu.

Uamuzi huo ulitolewa jana na Jaji Kiongozi Mustapha Siyani aliyekuwa anasikiliza kesi hiyo, ambapo mahakama ilikubali kuyapokea maelezo ya mshtakiwa anayedaiwa kukiri kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi.

Katika kesi hiyo Mbowe na wenzake watatu wanakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi na mashitaka ya kula njama na kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi kwa lengo la kuvuruga amani ya nchi.

Uamuzi wa mahakama kupokea maelezo hayo, umekuja baada ya mwezi mmoja wa mvutano wa kisheria kati ya wanasheria wa Serikali na wale wa utetezi waliokuwa wakipinga maelezo ya mshitakiwa wa pili, Adam Kasekwa yasipokelewa mahakamani kama kielelezo.

Mawakili wa utetezi walipinga kupokewa kwa maelezo hayo, wakidai kuwa mshitakiwa huyo aliteswa na kutishwa kabla ya kuchukuliwa maelezo akiwa polisi.

Hata hivyo, Jaji Siyani alitupilia mbali mapingamizi ya utetezi akisema yalikosa mashiko ya kisheria na kukubaliana na hoja za Jamhuri kuhusu uandikwaji na uwasilishwaji wa maelezo hayo mahakamanikuwa ulikidhi matakwa ya sheria.

Soma zaidi: Mahakama yatupa mapingamizi kesi ya Mbowe, wenzake

Kupokelewa kwa maelezo hayo, kunamaanisha kuwa mahakama sasa inaweza kuyatumia maelezo ya kukiri kwake kosa pamoja na ushahidi mwingine wa mashtaka katika kuamua kesi hiyo. Uamuzi huo wa jana ulitokana na kesi ndogo iliyoibuka ndani ya kesi ya msingi ambayo Mbowe na wenzake wanashitakiwa kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi vikiwemo vya kulipua vituo vya mafuta na sehemu zenye mikusanyiko ya watu, kwa lengo la kuvuruga amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa 2020.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Oktoba 21,2021, Katibu Mkuu wa Chadema John Mnyika, amesema uamuzi uliotolewa madhara yake hayapo kwenye kutafuta haki ya Mbowe tu, bali inatengeneza mfumo, taswira na ushawishi kwa majaji wengine.

Soma zaidi:Utata waibuka alipo mtuhumiwa kesi ya kina Mbowe

Amesema uamuzi huo unakwenda kutoa mwanya kwa Jeshi la Polisi kutokamilisha upelelezi na kuendelea kuwashikilia watuhumiwa kwa zaidi ya saa nne kinyume na kifungu cha 50 na 51 cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai (CPA)

“Zipo sababu zilizokosewa katika kutoa uamuzi, Jaji hakuongozwa na wala kufuata misingi ya kijinai kutokana na kutodhibitisha ushahidi uliotolewa pasipo kuacha shaka,”amesema Mnyika.

Amesema sababu nyingine ni pamoja na watuhumiwa kuhojiwa nje ya muda uliowekwa kisheria, ambao unamtaka mtuhumiwa kuchukuliwa maelezo ndani ya saa nne kama kifungu cha 50 na 51 cha sheria kinavyoelekeza.

“Sababu nyingine ni Jamhuri kueleza kuwa, walizunguka na mtuhumiwa, ushahidi na vielelezo vilivyotolewa mahakamani, ni kwamba polisi waliandikisha maelezo ya wasichana wawili na kuwasainisha lakini hawakusema, hawakuwa na muda wa kuandikisha malezo ya mtuhumiwa kwa kuwa walikuwa wanamtafuta mwingine,” amehoji Mnyika.

Pia, ametoa rai kwa Mahakama akisema wakati inajiandaa kumpangia Jaji mwingine kuendesha kesi hiyo ni vyema kuzingatia mtu ambaye hawezi kuingiliwa. Hata hivyo, Mnyika hakuwa tayari kufafanuzi zaidi kauli yake hiyo.


Amesema Chadema bado kinasisitiza hakijafunga milango ya mazunguzo na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwa, Mbowe alikwishaandika barua kuomba kukutana naye tangu Aprili, mwaka huu.

By Fortune Francis 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments