DKT. TULIA ACKSON :BIBI TITI ATABAKI KATIKA HISTORIA YA NCHI

Na Khadija Kalili , Rufiji
Naibu Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa anatambua na kuthamini mchango wa  aliyekuwa  Mwenyekiti wa kwanza wa Jumuiya ya Wanawake  Tanzania (UWT) Hayati Bibi Titi Mohammed ambaye alikua  mwanachama namba 16 pia mpigania Uhuru alikua  mwanamke pekee atakayebaki katika historia ya kupigania Uhuru wa nchi ya Tanzania hivyo tukiwa tunaelekea kusherehekea miaka 60 ya Uhuru kumuenzi ni wajibu wa Kila mtanzania.

"Katika kusherehekea maisha  yake  Hayati Bibi Titi  tunatambua  mchango wake mkubwa ndani ya taifa hili na juhudi zake ndizo zilizo tufikisha sisi viongozi wanawake hapa  tulipo" alisema Naibu Spika Dkt. Tulia

Dkt. Tulia alisema  hayo alipozungumza katika mahojiano na  Michuzi Blog  kuwa hivi sasa nchi  imekuwa na viongozi wengi wa kike kutokana na hamasa za Bibi Titi  ambazo alizitoa kwa kina mama wa kitanzania  pamoja na  kina baba pia ambao alikuwa nao bega kwa bega  katika harakati za kudai Uhuru.

"Bibi Titi ni bibi yetu ni yeye  alisaidia  katika juhudi za kupigania Uhuru wa nchi yetu na kuhakikisha heshima yake inakuwepo hivyo na sisi  hatuna budi kumuenzi na kuthamini mchango wake"alisema Dkt. Tulia .

Tulipofikia sasa hivi mwanamke anaweza kujitambua kwani mwanamke ana uwezo wa kuweza  kufanya kazi  kama mwanaume na hili alilianzisha yeye enzi hizo kiwa kijana aliweza kufanya kazi began kwa bega na wanaume  hali ambayo ilimjengea Imani kubwa kwaaliyekuwa Rais wa Kwanza wa nchi hii Hayati  Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

Dkt. Tulia alisema kuwa kwa mustakabali huo wa sifa za ushupavu wa Hayati Bbi Titi viongozi wote wanaowajibu wa kuendeleza juhudi zilizoanzishwa na kufanyiwa na bibi Titi huku alisisitiza kuwa  nyayo hizo zinafuatwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Wakati huohuo alisema kuwa anaiomba serikali kuweka mkakati wa kuzalisha kina Bibi Titi  wengine  huku alifafanua namna ya kuwazalisha ni pale mwanamke anapopata fursa za. kazi wazitumie vizuri na kuweka rekodi katika ufanisi wa kazi.

 Akizungumzia kuhusu Jumuiya  ya Wanawake Tanzania (UWT),kuamua kilele chake kufanyika Ikwiriri Wilayani Rufiji Mkoa wa Pwani alisema kuwa  siku ya leo Oktoba 23   ni muhimu na siku kubwa katika bara la Afrika , ikumbukwe kuwa bibi Titi ni muasisi na katika enzi hizo  haikuwa jambo rahisi mwanamke kujitokeza hadharani na  kupambania kile alichokiamini kuwa ni haki  yake lakini yeye alipambana hadharani bila woga.

Aidha Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Pwani Mama Salma Kikwete alisema.kuwa  maadhimisho ya wiki ya UWT Taifa  kufanyika Rufiji ni jambo ambalo limempa faraja kubwa huku alisisitiza kuwapa vipaumbele  watoto wa kike bila.kuwasahau watoto wa kiume kwani na wao wana uhitaji hivyo  ni wajibu wote kupewa  malezi mazuri ikiwemo kuwapa Elimu ya kutosha Ili wote kwa pamoja waweze kutimiza ama kufikia njozi zao katika maisha.

Alisema  wakati alipokuwa Mwalimu aligundua kuwa wanafunzi wa kike wana usomaji na uelewa uliojaa changamoto nyingi ndipo alipopata fursa akaanzisha Taasisi ya WAMA huku lengo kubwa likiwa ni kumkomboa  mtoto wa kike kieleimu.

Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan aliyekuwa  mgeni rasmi katika kilele cha wiki ya UWT alimmwagia sifa   Bibi Titi kwa kusema kuwa  licha ya Leo kwamba anasifiwa lakini wakati akiwa anapigania uhuru na maslahi ya nchi kwa ujumla wapo watu ambao walimbeza na kumkejeli lakni yeye alikuwa mwanamke shupavu Kamwe yale maneno hayakuweza kumrudisha nyuma na kufifiza harakati zake.
Kwa mantiki hiyo basi amewataka wataalamu wa Uandishi wa historia waweze kuketi na kuandika masuala yenye historia za nchi Ili kuweza kusaidia Kizazi kijacho kutambua historia ya nchi Yao ikiwemo wanaharakati mbalimbali ambao waliweza kuchangia kuleta uhuru wa nchi akiwemo Bibi Titi Mohammed.

Rais  Samia alitoa wito kwa UWT kuongeza miradi  mingi Ili waweze kujitegemea, pia alisema amezisikiliza changamoto walizonazo hivyo atakaa na viongozi watajadili kwa pamoja namna ya kuweza kuzitatua huku alisisitiza wanawake kushikamana na kuacha tabia ya kuchochea chuki miongoni mwao katika maeneo mbali mbali ikiwemo maeneo ya kazi kuacha makundi  huku akiwataka kushikana na kuwa walezi  bora wa familia kwa ujumla.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments