ISHU YA FAINI KUTOKA CAF, YANGA YAGOMEA YAKATA RUFAA

 


SHIRIKISHO la Soka Afrika, (Caf) limeipiga rungu ya faini ya milioni 11 Yanga kutokana na kile kilichoelezwa kuwa kufanya fujo kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Rivers United pamoja na kuingiza mashabiki kwenye mchezo huo.

Ikumbukwe kwamba Septemba 12, Uwanja wa Mkapa baada ya dakika 90 kwenye mchezo wa awali ubao ulisoma Yanga 0-1  Rivers United, ilielezwa kuwa wapinzani hao wa Yanga walipeleka malalamiko Caf kuwa walifanyiwa vurugu pamoja na uwepo wa mashabiki kwenye mchezo ambao haukupaswa kuwa na mashabiki.

Taarifa kutoka Caf imeeleza kuwa Yanga walishindwa kujibu taarifa za tuhuma hizo za kuwafanyia fujo watu waliokuwa kwenye msafara wa Rivers United ya Nigeria pamoja na kubaini uwepo wa mashabiki uwanjani.

Akizungumza na Championi Jumatano,Mkuu wa Idara ya Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli aliweka wazi kuwa walipata barua hiyo ila wameshangazwa na hukumu hiyo jambo ambalo limewafanya wakate rufaa.

“Tulipokea barua Oktoba 5 na tulipaswa kuijibu, kabla hatujaijibu adhabu imetolewa, sababu ambazo zimetajwa tunaona kwamba ni suala la mashabiki hilo lipo chini ya Shirikisho la Soka Tanzania, (TFF) sisi Yanga hatuhusiki na kwa upande wa vurugu ilikuwa ni stewart ambao wanasimamia hivyo tumewaandikia barua Caf kukata rufaa juu ya suala hilo,” alisema Bumbuli.


Post a Comment

0 Comments