Recent-Post

Jamii Yatakiwa Kuacha Kutamani Mambo Yaliyo Nje Ya Uwezo Wa Hali Zao Za Kimaisha Kuepuka Msongo Wa Mawazo

 Katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo msongo wa mawazo, Jamii imetakiwa kuacha kutamani mambo yaliyo nje ya uwezo wa hali zao za kimaisha.


Wito huo umetolewa na  Mwenyekiti wa chama cha Ugonjwa wa Kisukari ambaye pia ni Mwenyekiti wa shirikisho la magonjwa yasioambukiza Prof. Andrew Swai, wakati wa kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za Sekondari lililoratibiwa na wataamu kutoka Wizara ya Afya kuhusu magonjwa yasiyoambukiza katika shule za Muungano na Ishupu mkoani Arusha.

Prof. Swai amesema baadhi ya watu wamekuwa wakipatwa na tatizo la msongo mkubwa wa mawazo kutokana na kutamani kufanya mambo yaliyofanywa na watu wengine wakitambua kuwa hali zao haziruhusu.

Aidha, Prof. Swai amesema, miongoni mwa sababu inayochangia watu wenye magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo kisukari kutopata matibabu ya moja kwa moja na kufika sehemu za kutolea huduma za afya wakati tatizo limeshakuwa kubwa.

“Magonjwa yasiyo ya kuambukiza yamekuwa yakishamiri hivi sasa kutokana na mitindo ya maisha ambapo zaidi ya asilimia 9 ya watanzania wanaugua kisukari huku asilimia 6 wanaugua shinikizo la damu lililozidi”, ameeleza Prof. Swai.

Amesema endapo mtu atapima na kufahamu mapema kusumbuliwa na ugonjwa usioambukizwa anaweza kupewa ushauri wa matumizi ya vyakula na tatizo likaisha kabisa.

Kwa upande wake Mratibu wa Mradi wa Magonjwa yasiyoyakuambukiza kutoka TDA, Dkt. Rachel Nungu amesema miongoni mwa sababu zilizosababisha kujikita kutoa elimu kwa wanafunzi wa shule za Sekondari ni kuwajengea uwezo wakiwa bado wapo katika umri ambao wanaweza kujiepusha na vitu vinavyoweza kuwasabishia magonjwa yasiyoambukiza.

Waziri Ndonde ambaye ni mtaalamu wa afya na mazoezi amesema pamoja na shughuli za kimasomo wanazofanya wanafunzi hao, wamewaelimisha kutoa kipaumbele cha kuushughulisha mwili kupitia mazoezi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

Naye Mwalimu Wiliam Manyama ambaye ni makamu Mkuu wa shule ya sekondari Ishupu amesema, wanafaunzi wa shule yake wamepata elimu ya kutosha juu ya kukabiliana na magonjwa hayo huku akiishukuru Wizara ya Afya kwa kuona umuhimu wa kutembelea jamii mpaka maeneo ya vijijini.

Akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wa shule ya Sekondari Ishupu Vicent Mosha, pamoja na kutoa shukrani zake kwa wataalamu hao kwa kutoa elimu hiyo, ameomba utaratibu wa utoaji wa elimu hiyo uwe endelevu ikiwezekana iwafikie mpaka wazazi na walezi majumbani.Post a Comment

0 Comments