Recent-Post

KABAKA AKABIDHI MASHUKA 100, TAULO ZA KIKE 2500 WILAYANI RUFIJI

KUELEKEA kilele cha maadhimisho ya wiki ya UWT kitaifa kesho Oktoba 23, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Gaudentia Kabaka ametembelea Hospitali ya Wilaya ya Rufiji na kukabidhi mashuka 100 sambamba na kukabidhi taulo za kike 2500 kwa Shule ya Sekondari Utete na Ikwiriri.

Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo, Mwenyekiti Kabaka amesema UWT ni Jumuiya ambayo imekua ikiunga mkono jitihada za Serikali katika sekta mbalimbali hivyo katika kuadhimisha kilele cha wiki yao wameona ni vema wazifikie jamii na kukabidhi misaada yao hiyo.

Kabaka amewataka wanafunzi wa kike kusoma kwa bidii ili kuunga mkono juhudi na jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan ya kuboresha sekta ya elimu na kuwainua Wanawake nchini.

Amewataka wanafunzi hao kujilinda na mimba za utotoni na kuepuka kukimbilia kuolewa kwani kufanya hivyo kutalinda heshima ya Rais Samia kwani na yeye ametokana na kundi la Wanawake.

"UWT Taifa tumefika hapa kuzungumza na nyinyi mabinti wa kike wasomi, tumewaletea taulo hizi zipatazo 2500 kwa shule hizi mbili za Ikwiriri na Utete ambazo naamini zitawasaidia kutatua changamoto zenu za kila mwezi za kimaumbile ambazo kwa namna moja ama nyingine huwazuia kuhudhuria masomo yenu.

Ziepukeni Ndoa za utotoni lakini pia msikubali kupata mimba ili muendelee na elimu na kuweza kufikia malengo yenu, tunaamini ndani ya kundi hili kuna akina Rais Samia wengi, kuna Mwenyekiti wa UWT na mawaziri wengi sana, someni Taifa linawategemea," Amesema Kabaka.

Mwenyekiti Kabaka ameishukuru Kampuni ya HC Pad Tanzania kwa kufanikisha mchango wa taulo hizo za kike ambapo amewataka kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kuwafikia wasichana wengi zaidi mashuleni.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka akikabidhi mashuka kwa uongozi wa Hospitali ya Wilaya ya Rufiji alipoitembelea Hospitali hiyo na kukabidhi mashuka 100.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka akimkabidhi mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Utete Wilayani Rufiji taulo za kike wakati alipofanya ziara katika Wilaya hiyo.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka akikabidhi msaada wa vyakula na mahitaji mengine kwa Watoto wa Kituo Cha Watoto wenye uhitaji Wilayani Rufiji.

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari Utete iliyopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani.

Wanafunzi wa Shule ya Sekondari Utete iliyopo Wilayani Rufiji Mkoani Pwani wakimshangilia Mwenyekiti wa UWT Taifa, Gaudentia Kabaka alipofika kuzungumza nao leo.

 harles James

Post a Comment

0 Comments