Kina Mkude msituzingue kabisa

 

SIKU kadhaa zilizopita staa wa Simba, Jonas Mkude aliondolewa kwenye timu ya Taifa. Ilielezwa kwamba alikuwa na matatizo ya kifamilia lakini saa chache baadae akaonekana kwenye mazoezi ya Simba.

Ni jambo ambalo lilishtua wengi lakini ikaja kubainika kwenye benchi la ufundi kwamba kuna jambo la utovu wa nidhamu ambalo alilifanya wakati anaingia kambini ambalo Kocha Kim Poulsen hakutaka kuyakuza akamwambia aondoke ndio maana muda mchache badae akaibukia kwenye klabu yake ingawa nako huko baadhi ya viongozi siku hiyo walikuwa wakinyoosheana vidole ingawa hakuna aliyetaka kufungua mdomoni kuzungumzia waliyoyaona kwa staa huyo.

Ninataka kusema nini. Wachezaji wetu wajifunze kuheshimu kazi. Wasituzingue. Wajue umuhimu wa kazi yao na waweke mbele masilahi ya Taifa sambamba na kujitambua ili watoke hapo walipo. Wasiridhike na hizi siasa na Simba na Yanga, mpira wa sasa una pesa nyingi.

Wachezaji wetu wakubali kubadilika na kuendana na kasi ya dunia ya sasa na kuachana na mambo ya kukariri kama walivyokuwa wamezoea enzi za nyuma. Lazima wajifunze kuzingatia misingi na nidhamu ya kazi ndani na nje ya uwanja ili kuepukana na aibu kama hizo za kuondolewa kambini.

Sisi mashabiki huku mtaani tunajua. Ili mchezaji kama Mkude na wale waliosimamishwa kimyakimya pale Azam wafanikiwe binafsi lazima uwe na nidhamu ya kazi na uwaheshimu na wale wanaokuzunguka kwenye utendaji wako.

Starehe zipo lakini zisiharibu utaratibu wa kazi na maisha ya kila siku ya mchezaji. Kila jambo liwe na kipimo na kiwango chake.

Huwezi kujiamulia kufanya mambo kienyeji ukadhani kwamba utafanikiwa, nidhamu ya kazi haswa kwa mchezaji mkubwa mzawa ni kitu cha msingi sana kwavile inamsaidia kujijenga ndani na nje ya uwanja.

Na vilevile tunaamini mchezaji wa Ligi Kuu kwa Simba au Azam na wachezaji wengine wa aina yake wanapaswa kubadilika na kuwa mfano kwa wachezaji chipukizi ambao tunaamini kwamba wanatamani siku moja wangekuwa na kiwango kama chao.

Nidhamu ya kazi ndiyo itakayomsaidia mchezaji kuimarika mazoezini pamoja na kwenye mechi uwanjani,huwezi kuwa fiti kimchezo kama huna nidhamu kambini ambayo inakwenda moja kwenye suala la kuwahi pamoja na kufuata maelekezo yote.

Ndio maana wachezaji wengi wanashindwa kuhimili mikiki ya mashindano makubwa na klabu zao au na timu za Taifa kutokana na kutozingatia mambo ya msingi.

Hii wakati mwingine inaweza kuwa ni athari au matokeo ya moja kwa moja ya kutoheshimu mazoezi au nidhamu ya maelekezo ya viongozi mbalimbali wa ufundi na hata kutokuwa na utaratibu kwenye maisha ya kawaida.

Tunaamini mafanikio yao ndani ya klabu yatakuwa na athari chanya pia kwenye kikosi cha Taifa Stars kwavile atakuwa bora na mchango wake utaboreka zaidi kwenye mashindano mbalimbali. Hivyo ni wakati wa wachezaji wetu kujituma zaidi na kufuata maelekezo ya benchi la ufundi wanapokuwa ndani na nje ya uwanja kuliko kujiona kwamba wameshafikia kilele cha mafanikio kwa kusifiwa huku Sinza au pale Kwa Mkapa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments