Kwa mbinu hizi Yanga itafunga sana

KUIMARIKA kwa Yanga katika maeneo matatu kimbinu ya kupika mabao, kumeifanya timu hiyo kuonekana tishio kwa safu ya ulinzi ya timu pinzani katika siku za hivi karibuni kulinganisha na msimu uliopita.

Tofauti na msimu uliopita, Yanga ilikuwa na wakati mgumu katika kutengeneza nafasi za mabao, mambo yanaonekana kuwa tofauti msimu huu na hilo limejidhihirisha katika mechi tatu za Ligi Kuu ilizocheza hadi sasa.

Maeneo matatu Yanga iliyoonekana kuimarika ambayo kimsingi ndio yanaweza kuifanya timu iwe tishio au dhaifu katika ujenzi wa mashambulizi ni uimara wa namba (idadi), uimara wa ubora na uimara wa nafasi

Katika mechi tatu za Ligi Kuu ilizocheza dhidi ya Kagera Sugar, Geita Gold na KMC, nyota wa Yanga wameonyesha ufanisi mkubwa katika kuwepo katika nafasi sahihi pindi wanapoelekea langoni mwa adui, ubora wa kumzidi ujanja adui na kuingia kwa idadi kubwa au sawa na ya walinzi kwenye eneo la hatari la timu pinzani pindi wanaposhambulia.

Ushahidi wa hilo ni mabao manne iliyoyafunga katika Ligi Kuu hadi sasa na kila moja limeonekana kuchangiwa na kuimarika kwa Yanga katika mambo hayo matatu ya msingi pindi timu inapotengeneza shambulizi. Bao pekee Yanga ililolipata dhidi ya Kagera Sugar kwenye mechi ya kwanza, lilitokana na uimara wa Yanga kinafasi na kinamba pale ilipokuwa inashambulia.

Yacouba Songne alipoupora mpira kutoka kwa Erick Kyaruzi alimpasia Fiston Mayele aliyesimama katika nafasi nzuri ambayo hakuwa amekabwa na beki yoyote wa Kagera na hata shuti lake lilipopanguliwa na kipa Ramadhan Chalamanda, mpira huo ulitua miguu mwa Feisal Salum ambaye naye alikuwa hana bughudha ya mabeki na kuujaza wavuni kuandika bao hilo.

Wakati huo, kwenye boksi la Kagera Sugar, kulikuwa na wachezaji watatu wa Yanga, Yacouba, Feisal na Mayele sawa na namba ya walinzi wa Kagera Sugar waliokuwa ni Kyaruzi, Abdallah Mfuko na Jackson Kibirige.

Katika mchezo dhidi ya Geita Gold, bao pekee la ushindi la Yanga lilitokana na uimara wa ubora ambao ni matokeo ya ufundi wa mchezaji kumpiku beki au mlinzi wa timu pinzani pindi timu yake inaposhambulia.

Yacouba alipopokea pasi ya Kibwana Shomary akiwa pembeni ya uwanja, aliwahadaa walinzi wawili wa Geita Gold na kulazimisha kuingia katika eneo la hatari la wapinzani wao na kisha kupiga pasi nzuri kwa Ducapel Moloko aliyeujaza mpira wavuni,

Moloko alifunga bao hilo akinufaika na mkimbio mzuri alioufanya kuwahi katika nafasi nzuri ambayo pasi hiyo ya Yacouba ilimkuta na hakufanya ajizi kuipatia timu yake bao.

Hilo limejitokeza tena katika mabao ambayo Yanga imeyapata katika ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya KMC mjini Songea juzi.

Bao la kwanza la Mayele lilichangiwa na nafasi nzuri ambayo mshambuliaji huyo alisisimama katikati ya walinzi wawili wa KMC, pindi alipounganisha shuti la Feisal na kumpoteza uelekeo kipa Farouk Shikhalo na kuiandikia timu yake bao la kwanza.

Kocha wa KMC, Ahmad Ally alikiri makosa ya wachezaji wake kutoziba mianya kwa wachezaji wa Yanga ndio yalichangia wapoteze mechi hiyo

“Ni makosa ambayo yamefanywa na wachezaji wangu ambayo wapinzani wetu waliweza kuyatumia. Makosa hayo yalikuwa kwenye eneo la ulinzi na kiungo ambayo wenzetu walitumia na kupata mabao,” alisema kocha huyo. Lile la pili ambalo lilifungwa na Feisal Salum lilitokana na muunganiko wa vitu viwili ambavyo ni uimara katika kuwepo kwenye nafasi sahihi kwa wachezaji wa Yanga lakini pia uimara wa mchezaji kuwazidi ujanja walinzi wa timu pinzani.

Yacouba Songne alionyesha ubora wa kuwahadaa walinzi wa KMC na kupiga pasi ya kupenyeza kwa Fiston Mayele ambaye alimtengea Feisal Salum aliyekuwa katika nafasi nzuri iliyomwezyesha kupiga shuti lililojaa wavuni.

Kocha Nabi alisema timu yake inaonyesha kufanyia kazi kile ambacho amekuwa akiwaelekeza wachezaji na anaamini ubora walioonyesha utaendelea kuwepo.

Nyota wa zamani wa Yanga, Mohamed Hussein alisema ana imani kubwa mabao mengi yatafungwa na timu hiyo msimu huu.

“Safari hii tuna kikosi kizuri na tuna wachezaji wanaojua nini wanachotakiwa kufanya ndani ya uwanja hivyo huo ni mwanzo tu naamini mambo mazuri yanakuja,” alisema.

Kocha wa Yanga, Nasreddine Nabi alisema watahakikisha wanalinda na kuboresha zaidi ufanisi wao katika kushambulia ili wafanye vyema katika mechi zinazofuata.

“Kitu kikubwa tunataka tuboresha na kuimarika ili tuwe na mwendelezo huu ubora katika dakika 90 kwani kuna wakati tunaonyesha kupungua,” alisema Nabi.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments