Recent-Post

Mbunge ashikiliwa, ahojiwa kwa saa tatu, atuhumiwa kichapo kwa Katibu UVCCM

 George Mwanisongole ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Mbozi mkoani Songwe ameshikiliwa na kuhojiwa kwa zaidi ya saa tatu katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Vwawa wilayani Mbozi.

Mheshimiwa huyo amehojiwa kwa tuhuma za kuhusika na tukio la kushambuliwa kwa kipigo alichofanyiwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Wilaya ya Mbozi Ignas Kinyoa, majira ya saa 5:00 asubuhi katika eneo la Ichenzya mjini Vwawa.

Aidha, kupigwa na kujeruhiwa vibaya katibu huyo na kupelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Songwe iliyopo Vwawa kumehusishwa na tukio la kuchomwa gari la mbunge huyo lililotokea Septemba 29, mwaka huu.

Janethi Mngomi ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe jana Oktoba 3, 2021 amesema kuwa, alipigiwa simu na mbunge akimjulisha kuwa vijana wa UVCCM wamemkamata kijana mmoja anayedai amekuja kupeleleza tukio kuchomwa gari la mbunge.

Kufuatia tukio hilo la kupigwa katibu huyo, Jeshi la Polisi limemhoji Mbunge wa Mbozi, Mwenisongole, mtumishi wa NIDA, Kambi Kondo na Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya kutwa ya Vwawa, Godfrey Dunda.

Amesema, mbunge huyo alimweleza kuwa kijana huyo ambaye ametokea Malinyi mkoani Morogoro mbali na kwamba ni kada wa UVCCM, lakini amejitambulisha kuwa ni mganga wa kienyeji.

"Baada ya kupewa maelezo hayo na mbunge nilimpa maelekezo Mkuu wa Upelelezi Mkoa ili aanze kufuatilia na bahati mbaya RCO alipomtafuta mbunge kwa simu hakupatikana," amesema.

Kamanda Mngomi amesema saa 6:00 mchana alipokwenda ofisini kwa shughuli za kikazi alimkuta Katibu wa UVCCM wilaya Mbozi, Kinyoa akiwa amekalishwa kaunta huku akionekana amepigwa na kuvimba uso.

"Nilitoa maelekezo apewe PF3 aende kutibiwa na nikamuona kijana mwingine aliyedaiwa kwenda ofisi za UVCCM ambaye pia nilimhoji naye alikuwa amepigwa, kwa hiyo nikaagiza wote wapewe PF3 wakatibiwe,"amesema.

Ameongeza kuwa, baada ya kutibiwa na kurejea polisi, alimuuliza Katibu wa UVCCM amepigwa wapi na nani akajibu nusu saa iliyopita alipigiwa simu na mbunge kwamba yeye Katibu anahitajika polisi.

Kamanda Mngomi amesema kwa mujibu wa katibu huyo baada ya kuelezwa hivyo na mbunge alianza kutafuta bajaji ili aende polisi, lakini akamuona mbunge amejitokeza akiwa na vijana watatu ambao ndio walimvamia na kumshambulia kwa kipigo.

"Kwa kuwa yeye Katibu wa UVCCM ndio alikuwa amepigwa,hivyo niliagiza afungue kesi dhidi ya vijana hao ambao alidai anawatambua," amesema.

Pia Kamanda huyo ameongeza kuwa, kijana mwingine, alipoulizwa alijibu ametokea Malinyi yeye ni kada wa UVCCM na ni mganga wa kienyeji amefika Mbozi kwa ajili ya kupeleleza tukio la kuchomwa gari la mbunge wa Mbozi,Mwenisongole.

Kamanda Mngomi aliagizwa aitwe mbunge naye ahojiwe ambapo mbunge huyo katika maelezo yake alisema siku moja kabla ya tukio la kuchomwa moto gari lake kijana anayedai ni mganga wa kienyeji alimpigia simu na kujitambuliwa kuwa ni kada na green guard ametokea Malinyi-Ulanga amekuja kusaidia kupeleleza garu lililochomwa.

"Mbunge alimuuliza kijana huyo namba zangu umepewa na nani akajibu na Katibu wa UVCCM aliyepigwa,"amesema.

Kamanda Mngomi amesema, polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kuhusiana na kijana huyo anayedai ni mganga wa kienyeji.

Katika hatua nyingine UVCCM Mkoa wa Songwe imetoa tamko la kulaani kitendo cha kuvamiwa, kupigwa na kudhalilishwa kwa katibu wa umoja huyo wilaya ya Mbozi, Ignas Kinyowa.

Mwenyekiti wa UVCCM mkoani Songwe, Andrew Kadege amesema hatua kali zichukuliwe kwa wote waliohusika. Kwa nyakati tofauti wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, kitendo hicho kimewashushia heshima kubwa, hivyo jeshi la polisi lifanye uchunguzi w akutosha ili waliohusika wawajibike haraka.

Post a Comment

0 Comments