Recent-Post

Mo Dewji: Tanzania salama kwa uwekezaji

Mwenyekiti wa kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL), Mohammed Dewji (Mo) amepongeza sera za Rais Samia Suluhu Hassan, akisema kwamba zitaimarisha na kukuza uchumi kwa kiwango kikubwa. Pia, amesema Tanzania ni salama kwa uwekezaji kwa kuwa, Serikali imeweka mifumo bora na ya wazi.

Mo alisema wawekezaji na wananchi wa kawaida wanauona mkakati wa Serikali kupambana na ugonjwa wa Uviko-19 na kuimarisha miundombinu muhimu ambao huko mbele, unaweza kuchochea kasi ya kukua kwa uchumi na kufika kati ya asilimia sita na saba.

“Tanzania tunaye Rais wa aina yake, anaitwa Samia Suluhu Hassan. Tunao wawekezaji wengi kutoka nje ingawa tulikwama kwa muda katika uwekezaji lakini mambo yamebadilika sasa hivi. Mabadiliko aliyofanya yataimarisha uchumi,” alisema Mo alipohojiwa na kituo cha runinga cha CNN akiwa Dubai nchini Falme za Kiarabu.

Alisema mapambano yameimarishwa, kwani juhudi za makusudi zilichukuliwa kuongeza uzalishaji wa barakoa na vitakasa mikono na sasa wananchi wanapata chanjo nchini kote.

Kutokana na athari za Uviko-19, uchumi wa Tanzania unakadiriwa kukua kwa wastani wa chini ya asilimia tano kwa mwaka

Kupitia kampuni yake ya MeTL inayoajiri zaidi ya wafanyakazi 34,000 katika mataifa 11 inakofanya biashara, Mo alisema amewekeza mamilioni ya dola kwenye kilimo cha katani na kuanzia mwakani MeTL itakuwa kampuni namba moja kwa uzalishaji katani Afrika na duniani kwa ujumla.

Kuhusu biashara kwa ujumla, Mo alisema kuna soko kubwa la bidhaa hasa za viwandani Afrika ambalo mwanzo lilitawaliwa na kampuni za kimataifa, ila sasa hivi wazawa wanajitahidi kukidhi mahitaji ya wananchi.

Alisema kwa sasa MeTL inauza bidhaa zake eneo la Afrika Mashariki na Kati, lenye zaidi ya watu milioni 350, huku mpango uliopo ukiwa ni kuenea barani kote

“Tumewekeza mamilioni ya fedha kwenye teknolojia na tunajitahidi kusambaza bidhaa zetu. Kwa sasa tunauza takriban chupa bilioni moja za vinywaji kwa mwaka, kuna ushindani kwenye bei,” alisema na kuongeza kuwa hana mpango wa kurudi kwenye siasa zaidi ya kujikita kwenye biashara.

Post a Comment

0 Comments