NAWAKUMBUSHA WACHEZAJI WAZALENDO, WAKATI UMEWADIA SIO MWISHONI


MOJA ya timu ambayo imekuwa gumzo katika usajili wake kwa ajili ya msimu ujao ni Mtibwa Sugar ya Turiani mkoani Morogoro.


Gumzo linatokana na Mtibwa Sugar kuonekana wamebadilika na kuachana na ule mfumo wa kusajili wachezaji makinda ambao wamekuwa wakiwakuza na baadaye kufaidika kwa kuwauza katika klabu mbalimbali nchini.


Safari hii, Mtibwa Sugar wanaonekana wameamua “kazikazi”, maana wanasajili kikosi kwa ajili ya kushindana katika Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho. Hata kama watakuwa wameanza ligi vibaya lakini kuna nafasi ya kufanya vizuri.


Ligi ndiyo imeanza, ni mapema sana kusema nani kashinda aukashindwa kufanya vizuri kwa kuwa ligi inazunguka kwa muda mwingi sana.

Inawezekana Mtibwa watakuwa tofauti na mbele watafanya vizuri. Kikubwa kinahitajika ni kuendelea kurekebisha kila kinachoonekana kilikuwa si sahihi.

Tuachane na Mtibwa Sugar, ninachotaka kulenga zaidi ni kwamba tumeona Ligi Kuu Bara ndio imeanza na mengi yanaanza kutengenezwa na majibu yatapatikana siku ya mwisho ambako kila mtu atakuwa akipiga hesabu zake.

Wachezaji wazalendo wameshindwa kufanya vizuri katikamsimu uliopita na hakika wageni walitawala kwa kiasi kikubwa na wakapata mafanikio makubwa kwa kiasi kikubwa.

Vigumu kuelezea kwa wepesi, mfano ukiona mfungaji bora ni John Bocco lakini utaona karibu yake waliofunga mabao mengi zaidi ni wageni na hata waliofanya vizuri katika ligi kuu zaidi ni wageni.

Wageni ndio wachezaji wameipa sifa Ligi Kuu Bara kwa kuuzwa kwa bei kubwa zaidi wakitokea Simba na Yanga. Na unaona wale waliouzwa wameuzwa katika ligi kubwa zaidi Afrika za Morocco na Misri.

Idadi ya wazalendo ni zaidi ya asilimia 80 kwa wageni walio katika ligi kuu lakini jiulize kwa nini mafanikio yao yanakuwa ni makubwa kwa zaidi ya asilimia 90 zaidi ya wazawa ambao ni wengi zaidi.

Hata katika vikosi vya Yanga, Simba na Azam FC, wageni ndio wanatawala zaidi katika vikosi vya kwanza. Jiulize, hatuna wazawa wenye uwezo kama hao wageni wanaotokea Zambia, Mali au DR Congo hata Burundi tu!

Basi huu ndio wakati mwafaka wa wachezaji wazalendo kuanza kujipima na wajue utakapofika mwisho wa msimu kutakuwa na suala la hesabu nini kimepatikana.

Kama huu ndio mwanzo na ndio ligi imeanza, wachezaji wazalendo wanapaswa kujua umefikia wakati wa kubadilisha mwenendo na kushindana. Ligi ndio imeanza na hii iwe kuanzia mechi ya kwanza badala ya kusubiri mwishoni.

Isije ikawa mwisho kabisa ndio linaanza suala la hesabu kwamba vipi inawezekanaje wageni wanaendelea kutamba.

Hakuna ubishi, kama mfungaji bora akawa mzalendo tena, beki bora, kiungo bora, kipa bora na ikiwezekana hata watoa pasi au waliookoa wawe wazalendo kwa kuwa wingi wao wanaweza kuonyesha huo ubora.

Lazima wachezaji wazalendo wajue ligi yao ni sehemu yao ya kuwasaidia kupanda na kufanikiwa kufanya vizuri na ikiwezekana kupata nafasi ya kwenda mbele kimaendeleo.

Wazawa wanapaswa kuona haya au aibu na haya mambo ambayo yanawafanya waonekane wa kawaida sana.

Ushindani sahihi ni sehemu ya kuwafanya watu wakue zaidi,wafanikiwe na wasonge zaidi na ikiwezekana wafanye bora zaidi. Wapi wazawa watafanya vizuri zaidi ya hapa kwao. 

Na kama watasubiri mwishoni mwa msimu ufike, basi kila msimu utaishia wao wakiwa wanaburuza mkia.

Imeandikwa na Saleh Ally

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments