Wasichana na watoto wa kike wana haki ya kuishi salama, kuelimika, kuwa na afya, sio tu katika miaka ya kulelewa, lakini pia wanapokuwa wamepevuka kuwa wanawake.
Hivyo basi ikiwa wanaungwa mkono vyema wakati wa miaka ya utotoni hadi ujana, wana uwezo pia wa kubadilisha ulimwengu.
Katika maisha yetu ya kila siku tunapofikiria kwa ujasiri kuwa tuko katika ulimwengu bora na salama kwa watoto wetu, hasa wasichana, watu wasio na nia njema wamethibitisha kuwa fikra hizo sio sahihi.
Watu hawa wanatuthibitishia kuwa vitendo vya unyanyasaji kwa watoto wa kike havijashuka kutoka angani, bali vinafanywa na watu wa karibu tulionao katika jamii zetu.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Kimataifa linaloshughulikia watoto (Unicef) Mkoa wa Shinyanga unaongoza ukiwa na asilimia 59, Tabora 55 na Mara asilimia 55 kwa ndoa za utotoni.
Ripoti hiyo ilieleza kuwa asilimia 31 ya wasichana nchini wanaolewa kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na asilimia tano kabla ya umri wa miaka 15.
Takwimu hizi zinaonyesha kuwa kunahitajika juhudi zaidi na ushirikiano kati ya Serikali, jamii na wadau ili kuhakikisha changamoto hii inakwisha.
Tanzania ikiwa moja ya mataifa ambayo yamejizatiti kupambana na changamoto za watoto wa kike, Oktoba 11 kila mwaka huungana na mataifa mengine kuadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani.
Katika juhudi hizo Serikali na mashirika mbalimbali huweka mikakati mbalimbali ya kujadili namna bora ya kukabiliana na changamoto hizo.
Moja ya mashirika yanayofanya vizuri katika kusimamia haki za watoto wa kike na wasichana ni Save the Children.
Shirika la Save the Children limeweka mikakati imara na thabiti ya kuhakikisha tatizo la ndoa za utotoni na zile za kulazimishwa linaondoka katika jamii zetu.
Moja kati ya matukio ambayo shirika hilo imeyafanya katika juhudi zake za kukabiliana na changamoto hiyo ni kuwaokoa wasichana kutoka katika adha hii.
Subira na Tatu ni wachache kati ya wasichana wengi ambao shirika la Save the Children llimewafikia na kuwasaidia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wasichana hao wamesilimulia ni kwa namna gani kwa kushirikiana na shirika la Save the Children waliweza kutoka kwenye tatizo hilo.
Subira
Subira ni msichana mdogo wa miaka 16, mzaliwa wa kwanza katika familia ya watoto watano na binti wa pekee kutoka Shinyanga. Binti huyo alikuwa kwenye wakati mgumu alipoambiwa kuwa anatakiwa kufunga ndoa na mwanaume tajiri ambaye umri wake ni mara tatu ya alionao yeye.
“Nilikuwa na umri wa miaka 15 tu wakati nilipoambiwa nifunge ndoa. Nilishtuka, nilimuuliza mama yangu kwa heshima huyu mtu ana umri gani? Alijibu miaka 25. Nilitilia shaka, nikapumua na kumnong’oneza “lakini mama sitaki kuolewa halafu mtu huyu anaonekana mzee hawezi kuwa na miaka 25”, mama alinibana kama ishara kwamba sipaswi kuuliza swali kwa sababu uamuzi unafanywa na wazee,” anaeleza Subira.
Alikiri kwamba mama yake alikuwa mkali sana kwake mara tu alipomwambia jaribio lake la kukataa pendekezo la kuolewa, lakini kwa Save the Children alielewa pole pole na hata kujaribu kumueleza mumewe juu ya jambo hilo, hata hivyo, juhudi zote hizo hazikuwa na faida yoyote.
Kwa ushawishi wa baba yake, walifikia uamuzi huo kwa kisingizio cha umaskini, hata hivyo, haikuwa sababu sahihi kwa binti yao kukubali kuolewa akiwa mdogo.
Lakini hata kabla ya hilo kutokea Subira kwa haraka aliripoti mpango huo wa familia yake kwa msimamizi wa kituo cha Save the Children alikopatiwa mafunzo. Shirika hilo na washirika wake walichukua hatua ya kuhusisha Jeshi la Polisi na kumuokoa Subira kutoka katika changamoto hiyo.
Kukataliwa kwa pendekezo hilo, ambalo lilifuta mpango wa ndoa moja kwa moja, kulisababisha manung’uniko mengi kutoka kwa wazazi wake. Kwa upande mwingine, kama ndoa hiyo ingefungwa ingekuwa na athari kubwa kwa mustakabali wa Subira, kwa sababu ingemnyima haki zake za msingi.
Baada ya kumaliza mitihani yake ya elimu ya msingi Septemba 2019, hakufanikiwa kuendelea na elimu ya sekondari na badala yake alikaa nyumbani kwa muda kabla ya kuanza kozi ya ushonaji chini ya kituo kilichoanzishwa na Save the Children kwa kushirikiana na washirika wake. Katika kituo hicho, Subira hakujifunza tu ushonaji bali pia elimu ya afya ya uzazi, stadi za maisha na kukabiliana na mila na desturi mbaya.
Tangu wakati huo, hajawahi kumuona baba yake lakini mara kwa mara huzungumza kupitia simu na kusema kuwa bado ni mkali na mkorofi. Hilo linamuumiza sana Subira lakini anaamini siku moja atarudi nyumbani na baba yake kujivunia yeye.
Kufuatia kutoweka kwa baba yake, Subira alikua mlezi wa familia licha ya ukweli kwamba alipaswa kuvumilia shida wakati mwingine. Alikuwa amefikia hatua ambayo angeweza kutengeneza nguo ili kupata kipato. Kwa sasa yuko tayari kufungua duka lake la ushonaji na kununua mashine moja ya ushonaji kutoka kwenye akiba yake. Ushonaji ni chanzo pekee cha kipato kwa familia yake kwa sasa tangu baba yake kukimbia.
“Kwa sasa lengo langu ni kumsaidia mama yangu kuendeleza familia hii. Pia nimemfungulia biashara ya matunda kwa hivyo mimi na yeye angalau tunaleta kitu mezani kwa pamoja, kwa njia hiyo ninaweza kuweka akiba kidogo kidogo ili niweze kutimiza ndoto zangu,” anaeleza Subira.
Maria (sio jina halisi) Mama yake Subira
“Kama mama na mke, nilikuwa kwenye wakati mgumu sana wakati mume wangu alipotaka Subira aolewe. Mimi mwenyewe niliolewa wakati nikiwa na umri miaka 13 tu. Kwa hivyo, chochote ambacho ningejaribu kumwambia juu ya athari za ndoa za utotoni nilikuwa mfano na angesema mbona wewe hakuna matatizo yaliyokupata mpaka leo,” anasema Maria.
Anasema, “Ninaamua kabisa kwamba kwa sasa maslahi ya binti yangu yanakuja kwanza. Wakati watu wa shirika la Save the Children walipokuja kuzungumza nami juu ya umuhimu wa kutomuozesha mtoto wangu, nilielewa vizuri na nikamwambia mume wangu kuwa Subira hataolewa, hakuwa na budi zaidi ya kusitisha ndoa hiyo. Kusema ukweli sikuwahi kutaka mume wangu akimbie lakini sikuwa na chaguo.”
“Kama mzazi, kwa sasa ninapinga kwa nguvu zote ndoa za utotoni kwani zinaharibu maisha ya baadaye ya wasichana na kuwaweka katika maumivu na majukumu mengi katika umri mdogo. Tuweke hadhi ya utu wa watoto wetu mbele na tutoe kipaumbele katika mafanikio yao,” anaeleza Maria.
Tatu
Tatu mwenye umri wa miaka 17, ni mama wa watoto wawili akiwa ameolewa miaka mitatu iliyopita. Mpango wa wazazi wake kutoka katika umaskini uliokithiri ulileta maumivu makali kwa msichana huyo kwani alilazimishwa kuolewa akiwa na miaka 14 kwa kubadilishana na ng’ombe 5.
Baada ya kumaliza elimu ya msingi, Tatu alikuwa nyumbani akiwasaidia wazazi wake kazi za nyumbani na shughuli za shamba wakati akingojea matokeo ya mitihani yake. Wakati huo huo mwanamume mmoja alitembelea nyumba yao na akaonyesha nia yake ya kumuoa Tatu. Hakuwa na lingine ila kukubali uamuzi wa wazazi wake wa kumuoza kwa nguvu na mwanaume ambaye alikuwa mara mbili ya umri wake.
“Wazazi wangu walitaka pesa, ng’ombe na zana za kilimo. Ilikuwa msimu wa mvua na matokeo ya mitihani hayakuwa yametoka lakini wazazi wangu waliamua kuniozesha. Hawakutaka ridhaa yangu, nilikuwa na huzuni sana lakini hakuna kitu ambacho ningeweza kufanya, ndoto yangu ilikuwa ni kuendelea na elimu ya sekondari,” anasema Tatu.
Tatu alikuwa na ndoto ya kuwa mwalimu na hii ilivunjika wakati alipochukua jukumu jipya la mama na mke katika umri mdogo. Mwaka 2018 alipata mtoto wake wa kwanza mvulana aliyeitwa Hamisi. Katika umri wake alijitahidi kumlea na akajikuta na mtoto wa pili mwaka mmoja baadaye. Akiwa hana ujuzi wa uzazi wa mpango na ufahamu wa afya ya uzazi, Tatu alikuwa katika hatari kubwa yeye na watoto.
“Bado nina matumaini. Nataka kuwekeza kwa watoto wangu. Nimefundishwa na Save the Children juu ya masuala ya afya ya uzazi, elimu ya kifedha, stadi za maisha na kutengeneza kipato kwa maisha endelevu. Mimi ni kinara wa jamii na ninaelewa umuhimu wa elimu na kwa nini tunapaswa kupiga vita ndoa za utotoni. Nitafanya kazi kwa bidii kuhakikisha kuwa watoto wangu hawaolewi mapema na kwamba wanamaliza shule na kutimiza ndoto zao,” anasema Tatu.
Tatu anapata riziki kutoka kwenye biashara yake ya mkaa na kutokana na mafunzo ya utunzaji wa fedha aliyoyapata kutoka Save the Children anatarajia kuipanua biashara hiyo. Amejifunza umuhimu wa kuweka akiba na anatarajia kukusanya pesa ifikapo mwisho wa 2021 ili kuanzisha biashara ya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa ili kuuza maziwa.
Maziku ambaye ni kinara wa jamii katika kupambana na ndoa za utotoni anasema “Tulipogundua kuhusu suala la Tatu, tulizungumza naye juu ya kumtoa kwenye changamoto hiyo lakini alifikiri ni bora abaki na baba wa watoto wake ili waweze kulea watoto hao pamoja. Hatukuwa na chaguo kwa sababu alisisitiza.”
“Tatu aliajiriwa katika timu ya vinara wa jamii, alifundishwa juu ya kusoma na kuandika, elimu ya kifedha, afya ya jinsia na uzazi, stadi za maisha na kukabiliana na mila na desturi mbaya ikiwa ni pamoja na ndoa za utotoni. Anapata huduma wakati wowote anapokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa pamoja na unyanyasaji kwani anaweza kuripoti kupitia nambari ya bure au dawati la jinsia la polisi. Yeye ni mmoja kati ya mabingwa mashuhuri wa jamii wanaotetea kuondoa ndoa za utotoni katika jamii yetu,” anaeleza Maziku.
Save the Children ilitekeleza mradi wa kiraia unaounga mkono juhudi kukabiliana na mila na desturi potofu mkoani Shinyanga kuanzia mwaka 2017 hadi 2019.
Lengo kuu la mradi huo lilikuwa ni kusaidia asasi za kiraia kupambana na mila, desturi na kanuni za kijinsia zinazowadhuru watoto na vijana, haswa wasichana waliovunja ungo.
Save the Children Tanzania pia wanashirikiana na asasi za kiraia kupitia mtandao wa Kukomesha Ndoa za Utotoni Tanzania kushinikiza marekebisho ya sheria ya ndoa ya 1971 ambayo inaweka umri wa chini wa ndoa kwa wasichana kuwa miaka 15 kwa idhini ya wazazi, 14 kwa idhini ya mahakama huku kwa wavulana ikiwa miaka 18.
Subira na Tatu waliokolewa kutokana na vitendo viovu na shirika la Save the Children kwa kushirikiana na wadau wengine kama vile Kiwohede kwani wao ni waangalizi wa haki za watoto ambao waliapa kuvunja utamaduni mbaya kupitia programu kadhaa za kujenga uwezo zilizotekelezwa.
Tukiwa katika maadhimisho ya siku ya kimataifa ya mtoto wa kike ni muda sahihi wa jamii, Serikali na wadau kuungana ili kuhakikisha suala la ndoa za utotoni linatokomezwa katika jamii yetu.
Siku ya kimataifa ya mtoto wa kike huadhimishwa Oktoba 11 kila mwaka na inazingatia hitaji la kushughulikia changamoto wanazokabiliana nazo wasichana na watoto wa kike kote duniani.
Siku hii imepangwa na Umoja wa Mataifa (UN) katika kuendeleza harakati za usawa wa kijinsia na kuongezea uwezo wa watoto wa kike pamoja na haki zao kama vile, haki ya elimu, haki ya kulindwa dhidi ya ubaguzi, haki za matibabu, kuepushwa na ndoa za utotoni na za lazima na haki nyinginezo. Pia siku hiyo huelezea mafanikio ya watoto wa kike na wanawake kwa jumla. Umoja wa Mataifa unasisitiza kuwa ndoa za utotoni ni moja ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu wanaofanyiwa wasichana katika mataifa mbalimbali duniani.
Hivyo ili kupambana nazo ni lazima kuwepo na ushirikiano wenye tija kati ya Serikali, mashirika ya kutetea haki za watoto, jamii na wadau wengine.
Ushirikiano huu utasaidia kupunguza kama sio kuondoa kabisa changamoto hiyo ambayo inaendelea kukandamiza haki za wasichana na watoto wa kike kote duniani.
0 Comments